SHAFFIH Dauda, mchambuzi wa masuala ya michezo na Mtangazaji amesema kuwa Yanga walipaswa kumpongeza mwamuzi wa kati Ahmed Arajiga na sio kuwa na mashaka naye.
Tayari kuelekea katika mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho kati ya Simba v Yanga, waamuzi wameshatangazwa huku wa kati akiwa ni Arajiga.
Mwamuzi huyo alichezesha robo fainali ya Simba v Dodoma Jiji nusu fainali Simba v Azam FC ambapo katika mchezo huu, Uwanja wa Majimaji alikubali bao la Luis Miquissone lililofungwa kwa faulo ya harakaharaka.
Kupitia kwenye ukurasa wao wa Instagram wa Yanga, jana Julai 22, Yanga waliandika waraka wa kutokuwa na imani na mwamuzi wa kati kwa kile walichoeleza kuwa amechezesha mechi nyingi za watani.
Dauda amesema:”Kuhusu mwamuzi tayari itakuwa ilipangwa tangu awali ni kama ilivyokuwa kwenye uwanja, ulijulikana kabla ya kujua nani na nani watacheza.
“Kwa kusema kwamba mwamuzi amechezesha mechi nyingi za watani hapo sioni tatizo, labda wazungumze kuhusu kiwango. Kwa hilo la mechi Yanga walipaswa wampe pongezi mwamuzi kwa kuwa amechezesha mechi mingi za mashindano haya.
“Ukiweka kando siasa moja ya waamuzi wazuri ni pamoja na Arajiga hivyo jambo la kuhoji ni kiwango na sio kusema amechezesha mechi na watani,”.
Fainali ya Simba v Yanga inatarajiwa kuchezwa Uwanja wa Lake Tanganyika Kigoma, Julai 25.