MSIMU wa 2020/21 kikosi cha Simba ambacho kimetwaa taji la Ligi Kuu Bara umeonekana kuwa bora kwao kwa kutawala katika takwimu nzuri.
Simba, licha ya kutwaa ubingwa wa ligi kuu msimu huu, ikiwa ni mara ya nne mfululizo lakini imeendelea kuonyesha kuwa ilikuwa ni timu tishio mara baada ya kufanya vizuri katika idara mbalimbali ndani ya uwanja na kuweka rekodi.
Simba katika ligi kuu msimu huu imefunga mabao 78 Yanga iliyo nafasi ya pili imefunga jumla ya mabao 52 na Azam FC iliyo nafasi ya tatu imefunga mabao 50.
Hii inatokana na wachezaji wa Simba binafsi kuonyesha viwango bora na kuwa na takwimu nyingi bora kuwazidi wapinzani wao Yanga pamoja na Azam FC.
Tukianzia katika orodha ya ufungaji bora wa ligi kuu msimu huu, Simba ndio inaongoza kwa kuwa na washambuliaji bora ambapo John Bocco ana mabao 16, Chris Mugalu mabao 15 na Meddie Kagere mabao 13.
Ni Prince Dube pekee kutoka katika klabu ya Azam FC mwenye mabao 14 ambaye ameweza kuwatingisha washambuliaji wa Simba, jambo ambalo linamfanya kuwa mmoja kati ya washambuliaji bora waliofanya vizuri msimu huu.
Rekodi hiyo imewekwa na wachezaji wa Simba pekee ya kuwa na washambuliaji watatu waliofunga mabao 10 na kuendelea na hakuna timu nyingine iliyofanya hivyo hata kwa upande wa Yanga na Azam ambazo ndio zimekuwa zikionyesha upinzani mkubwa zaidi kwa Simba.
Pia Simba imeonekana kuendelea kuwa bora mara baada ya kiungo wake Clatous Chama kuongoza katika orodha ya wachezaji waliotoa pasi nyingi za mabao โasistiโ akiwa ametoa jumla ya pasi 15 za mabao huku akifuatiwa na Luis Miquissone ambaye pia amepiga asisti 10.
Kwa upande wa Yanga na Azam hakuna mchezaji hata mmoja aliyefikisha idadi ya asisti 10 ambapo kwa upande wa Yanga ni Deus Kaseke mwenye asisti 6 na Iddy Nado mwenye asisti 9 ambao bado wamechemsha kuwafikia Chama na Luis.
Kwa upande wa makipa, bado Aishi Manula amefanya vizuri kulinganisha na makipa wengine alioshiriki ligi kuu msimu huu mara baada ya kufanikiwa kupata ‘clean sheets’ 18 huku Metacha Mnata wa Yanga akiwa na clean sheets 13, jambo ambalo linawafanya Simba kuzidi kutamba.
Ukuta wa Simba pia ndio uliofungwa mabao machache zaidi kuliko timu nyingine, ambayo ni 14 tu, wakati wanaofuata, Yanga umefungwa mabao 21 na Azam ni mabao 22.