Home Makala UKATILI WA AMBUNDO UWANJANI, NA STORI YA SAID BAHANUZI

UKATILI WA AMBUNDO UWANJANI, NA STORI YA SAID BAHANUZI


BAADA ya kukamilika kwa msimu wa Ligi Kuu Bara 2011/2012, kwenye dirisha la usajili la wachezaji wapya kulikuwa na jina moja ambalo lilitamba sana, hasa baada ya kugombaniwa na klabu zote kubwa hapa nchini za Simba na Yanga.

Jina hilo ni la mshambuliaji wa Mtibwa Sugar ya kipindi hiko, Said Bahanuzi ambaye alimaliza msimu huo akiwa amefunga mabao tisa.

Baada ya kukuru kakara za hapa na pale, Yanga ikashinda vita hiyo na kumsajili Bahanuzi kwa kwa ajili ya msimu wa 2012/13.

Licha ya kukiri kuwa alikuwa na hofu kubwa kutokana na ukubwa wa presha ya kuichezea Yanga, straika huyo alianza kwa kasi kwenye michezo ya kirafiki ya klabu hiyo kujiandaa na msimu mpya.

SOMA PIA : AMBUNDO: TUTAFANYA VIZURI, LEO YANGA KAZINI KWA MKAPA

Bahanuzi alianza kuonekana rasmi kwenye mechi za mashindano hasa Kombe la michuano ya Afrika Mashariki na Kati maarufu kama ‘CECAFA Kagame Cup’, ambapo mchezo wake wa kwanza ilikuwa ni dhidi ya Vital’O ya Burundi, akiingia dakika ya 78, na kuwa sehemu ya kikosi kilichoibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Kutokana na kiwango kikubwa alichokionyesha katika mchezo huo, Bahanuzi alifanikiwa kumshawishi kocha wa Yanga na kuanzia hapo michezo yote iliyofuata alianza kwenye kikosi na kucheza kwa dakika 90, ambapo alikuwa na moto kweli wa kufunga mabao.

Mashindano hayo ya Kagame ndiyo yaliyomng’arisha Bahanuzi kiasi cha kufanikiwa kuibuka mfungaji bora wa akiweka kambani mabao sita, mafanikio haya yalimfanya Bahanuzi awe miongoni mwa nyota waliozungumzwa zaidi na kutarajiwa kufanya mambo makubwa kwa msimu huo wa 2012/13.

Baada ya kuanza kwa Ligi Kuu msimu huo hali ilikuwa tofauti sana, ambapo nyota huyo alicheza michezo mitatu mfululizo ya kwanza bila kufunga bao.

Hali hii iliongeza presha kubwa kwa Bahanuzi ambapo zipo taarifa zinazoeleza kuwa kufuatia hali hii aliwekwa kitimoto na viongozi wa Yanga kwenye makao makuu ya klabu hiyo yaliyopo mitaa ya Jangwani, Dar es Salaam.

SOMA PIA JUMA MAKAPU WA YANGA KUIBUKIA MTIBWA SUGAR

Mara Bahanuzi akaanza kupigwa benchi huku akishutumiwa kwa vingi, ikiwemo kuhusudu starehe jambo ambalo mwenyewe alilikanusha.

SOMA NA HII  JINSI VITENDO VYA 'KISHOGA' VINAVYOZIDI KUSHAMIRI KWENYE LIGI KUU..WACHEZAJI , VIONGOZI WATAJWA...

Kibaya zaidi nyota huyo alikuja kukosa penalti ya ushindi dhidi ya Al Ahly ya Misri, kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo kama Yanga wangeshinda wangetinga hatua ya makundi ya michuano hiyo.

Hali ambayo ilizidi kumjengea uhasama na wadau mbalimbali wa Yanga wakiwemo baadhi ya viongozi na hata wachezaji wenzake. Kutokana na mazingira hayo   ilimpelekea aombe nafasi ya kuondoka na kwenda Polisi Moro, ambapo alifanikiwa kwa kiasi kurejesha makali yake kiasi cha kushinda tuzo ya mchezaji bora mara mbili.

Nimependa kurejesha stori hii ya Bahanuzi kwa kuwa, mimi ni miongoni mwa watu ambao wameguswa sana na uwezo mkubwa ambao umeonyeshwa na kiungo mshambuliaji mpya wa Yanga aliyesajiliwa kutokea Dodoma Jiji, Dickson Ambundo.

Ambundo alionyesha uwezo mkubwa kwenye mchezo wa ufunguzi wa michuiano ya kombe la Kagame dhidi ya Nyasa Big Bullets kutokea Malawi, ambapo alifanikiwa kutoa asisti ya bao lililofungwa na mshambuliaji Waziri Junior.

Hakuna ambaye hajui uwezo wa Ambundo na hiki ambacho anaendelea kukionyesha ni kitu ambacho kilitarajiwa na wengi, hasa kutokana na uwezo mkubwa aliouonyesha kwenye Ligi Kuu Bara msimu uliopita.

SOMA PIA :MANARA AMWAGA UGALI..AFUNGUKA A-Z KUHUSU BARBARA NA MO DEWJI MTAJA SENZO..

Nakumbuka mara baada ya kumalizika kwa mchezo wao wa mzunguko wa pili wa ligi dhidi ya Simba, kocha mkuu wa mabingwa hao watetezi aliweka wazi kuwa Ambundo ni miongoni mwa wachezaji wenye vipaji vikubwa, na walikuwa mwiba dhidi yao.

Bila shaka Ambundo amethibitisha maneno hayo ya Gomes, kwa kile alichokionyesha kwenye Uwanja wa Mkapa Jumapili iliyopita.

Kwangu nadhani Yanga wana kazi kubwa ya kumsaidia Ambundo kufikia katika kiwango cha juu na malengo yake kwenye soka, kwanza kwa kuhakikisha wanampa muda wa kuzoea mazingira na kupunguza presha kubwa dhidi yake, jambo ambalo ni wazi haliwezi kuwa rahisi kutokana na presha kubwa ya matokeo mazuri ambayo iko ndani ya kikosi hiko.

Lakini Ambundo mwenyewe anapaswa kutuliza kichwa na kuachana sifa anazopewa bali apambane kukuza kiwango chake.