Kikosi cha Young Africans kimeanza safari ya kurejea Tanzania kikitokea Morocco kilipokua kimeweka kambi.
Taarifa zilizotolewa na Mkurungezi wa uwekezaji wa GSM, Hersi Said ambaye aliambatana na kikoai cha Young Africans, zinaeleza kuwa mabingwa hao wa kihistoria katika soka la Bongo wamelazimika kusitisha kambi.
Hersi amesema wamelazimika kusitisha ratiba ya kambi yao ya nchini Morocco, kwa sababu zilizo nje ya uwezo wao, hivyo sehemu ya maandalizi yao wataikamilisha hapa nchini.
Amesema zipo sababu mbalimbali zilizowapelekea kufanya maamuzi hayo ila sababu kubwa ni wachezaji wao wanane kutakiwa kujiunga na timu za taifa kwa ajili ya michezo ya kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2022.
Wakiwa nchini Morocco, Yanga wameonekana wakifanya zaidi mazoezi ya kukimbia barabarani na Gym tofauti na wenzao Simba ambao bado wapo huko ambapo kocha wao Gomes amenza kuwapa mazoezi ya uwanjani.
Kikosi cha Young Africans kilitarajiwa kurejea nchini Ijumaa (Agosti 27), tayari kwa kilele cha wiki ya Mwananchi itakayofanyika Uwanja wa Benjamin Mkapa Jumapili (Agosti 29).