CAIRO, MISRI. MATUMAINI ya kocha Pitso Mosimane na timu yake ya Al Ahly kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Misri yamezimwa baada ya kutoka sare ya 3-3 dhidi ya El Gouna Jumanne, na kuishuhudia Zamalek ikitwaa taji hilo kutokana na ushindi wa 2-0 dhidi ya timu ya kiungo Mtanzania Himid Mao ya El-Entag El-Harby, ambayo imeshashuka daraja.
Kabla ya mechi, kulikuwa na matumaini madogo ya Ahly kutwaa taji lao ya 43 la ligi, wakitegemea ratiba iliyoonekana kwenye makaratasi kuwa ni nyepesi huku vinara Zamalek wakitarajiwa kudondosha pointi katika mechi zao.
Hata hivyo, matumaini hayo yalizimwa pale Zamalek a.k.a ‘White Knight’ walipopata ushindi mzuri wa nyumbani na kufanya matokeo ya Ahly yasiwe na maana yoyote.
Wakati wakihitaji pointi zote tatu – huku wakiombea Zamalek wadondoshe pointi, vijana wa Mosimane walisafiri kwenda El Gouna Stadium kukikabili kikosi cha kocha Reda Shehata.
Licha ya kutokuwa na cha kupoteza, El Gouna walipata bao la kuongoza katika dakika ya saba tu kupitia kwa Mohamed Naguib.
Goli hilo liliwaamsha mabingwa hao wa Afrika ambao walijaribu kila wewezalo, lakini walikumbana na ukuta wa chuma.
Kipindi cha pili, Al Ahly walipata cha kushangilia pale beki raia wa Tunisia, Ali Maaloul – ambaye alifunga bao kwa penalti iliyotokana na madhambi kwenye lango la El Gouna.
Dakika nane baadaye, Hussein El Shahat aliwatanguliza Al Ahly kwa mara ya kwanza pale alipofunga bao la pili akitumia asisti ya Amr El Solia.
Kikosi cha kocha Mosimane kiliandika bao la tatu kupitia kwa Mohamed Sherif katika dakika 82. Mara hii El Shahat ndiye aliyetoa asisti.
Hata hivyo, Vijana wa Jeshi hawakuwa tayari kufa kiahisi na wakapata bao lao la pili kupitia kwa Mahmoud Shabrawy akimalizia asisti ya Mcameroon, Jonathan Ngwem katika dakika ya 86.
Kisha wakapata penalti dakika za lalasalama ambayo alifunga Omar El Said na kulazimisha sare.
Ahly kukosa taji lao la 43 la ligi kunaweza kuzua maswali kuhusu kocha raia wa Afrika Kusini, Mosimane – ambaye alipewa jukumu la kuiongoza timu hiyo kutwaa mataji likiwamo la Ligi Kuu.
Mechi yao ya mwisho msimu huu wa 2020-21 ya kukamilisha ratiba Ahly watacheza dhidi ya Aswan Ijumaa.