Home BIashara United BAADA YA KUHAMIA YANGA NA KURUSHA VIJEMBE SIMBA…WANASAIKOLOJIA WAMTABIRIA HAYA MANARA

BAADA YA KUHAMIA YANGA NA KURUSHA VIJEMBE SIMBA…WANASAIKOLOJIA WAMTABIRIA HAYA MANARA


HABARI ya mjini kwa sasa ni Haji Manara. Kitendo chake cha kutua Yanga akitokea Simba, huku akiwa mmoja ya watu waliokuwa wakiwanyima raha Wanajangwani, imezua mijadala mingi nchini na kushangaza wengi.

Licha ya zama zilizopo sasa soka kuwa ni biashara na sio unazi, bado usajili wa Yanga dhidi ya Manara umekuwa kivutio sio kwa wadau wa soka tu, bali hata wanayanga wenyewe, ila baadhi ya wanasaikolojia wamefichua mambo yanayoweza kumuathiri Msemaji mpya huyo wa Yanga katika maisha yake mapya akiwa Jangwani alikotambulishwa hivi karibuni akitokea Msimbazi alikodumu kwa miaka saba mfululizo.

Usajili huo wa Manara Jangwani, licha ya kuwagawa baadhi ya wadau wa soka wengine wakimlaumu kwa uamuzi huo na wengine wakimpongeza huku baba yake mzazi, Sunday Manara akisisitiza alichokifanya kijana wake ni sahihi kutokana na kilichomfukuza Msimbazi.

Manara aliondoka Simba akitofautiana na baadhi ya viongozi wa juu wa Bodi ya Wakurugenzi wa klabu hiyo na wiki kadhaa baada ya kubwagana na Simba akatambulishwa Jangwani na tayari ameanza mbwembwe zake ikiwamo kuwapiga vijembe mabosi wake wa zamani na kuleta raha kwa wanayanga.

WASIKIE WANASAIKOLOJIA

Hata hivyo, Mwanasaikolojia Sukambi Deogratius amesema Manara ana nafasi ya kufanikiwa au kufeli na alivyozoeleka kulingana na changamoro atakazokutana nao katika ofisi yake mpya Jangwani.

Alisema changamoto itakayokutana nayo Manara Yanga ni mapokeo ya Wanayanga wote kama yatakuwa ni hasi au chanya kwa baadhi yao, na wakati huu bado yuko kwenye kipindi cha mpito.

“Kisaikolojia naamini hata kilichomchochea hadi kuhamia uko si uamuzi wake binafsi, kuna wengi walimshauri, kiukweli Haji ana maadui na marafiki pia, japo ni katika mazingira ya kimchezo.

“Namna atakavyokaribishwa na kupokelewa ndani ya klabu hiyo ndivyo vitaamua ustawi na salama wake kwenye timu aliyokwenda,” alisema Sukambi aliyeongeza kuwa, kisaikolojia halikuwa jambo jepesi kwa Manara kuhamia Yanga na kuna uwezekano mkubwa waajiri wake wapya walimuandaa sana kisaikolojia.

“Kuna vitu vingi moja kwa moja lazima alijiuliza, matamshi yake akiwa Simba, jina lake na hata hadhi yake na itakuwa amehakikishiwa vyote hivyo vitalindwa, ingawa kwa sasa bado yuko katika kipindi cha mpito. Ili awe sawa, itategemea na muitikio wa Wanayanga kwake, kama atapokelewa vizuri basi ndilo litathibitisha yuko huru na salama,” alisema.

SOMA NA HII  ALICHOSEMA EDO KUMWEMBE BAADA YA SIMBA KUWA KWENYE MPANGO WA KUWAACHA KAGERE NA MUGALU...

Alisema kama matarajio yakiwa tofauti na malengo kwenye timu hiyo, kisaikolojia itabadilika na atakuwa mgeni katika mazingira ya Jangwani na kama hatakuwa makini inaweza kumletea athari siku za usoni.

Kuhusu kukulia katika familia ya Yanga wakati wa utoto wake naye kuwa kinyume, mwanasaikolojia mwingine, Leons Maziku alisema kwa mtoto wa kiume, masuala ya imani au itikadi ya timu au chama uwa si shida kuwa tofauti na familia kama itakavyokuwa kwa mtoto wa kike.

“Katika saikolojia kwa mtoto wa kiume anapofika umri fulani huwa anafuata njia zake, hajisikii vibaya kutofautiana na mzazi kwa jambo ambalo anaona yeye yuko sahihi kulifanya. Mtoto wa kike mara nyingi atapenda kumfurahisha mzazi, ndio sababu kuna tofauti kubwa unapomwambia mtoto wa kiume asome kwa bidii atataka umuonyeshe kuna faida gani kwake atakaposoma kwa bidii kulinganisha na mtoto wa kike ambaye atasoma kwa bidii ili kuwafurahisha wazazi.”

Alisema ndivyo ilitokea kwa Manara, licha ya familia yake kuanzia baba yake mkubwa, Kitwana na mzazi wake, Sunday na ndugu zake wengine kuwa ni Yanga damu, yeye alikuwa ni mnazi wa Simba, akifuata nyayo za babu yake mzaa mama ambaye alikuwa ni Simba lialia naa kuiongoza kama Mwenyekiti wao.

Baada ya miaka saba akiwa Ofisa Habari wa Simba, Manara ni kama amefanya sapraizi kwa baadhi ya mashabiki wa timu hiyo na hata wale wa Yanga baada ya kutambulishwa Jangwani hivi karibuni, sasa leo ataonekana kwa mara ya kwanza kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa, Dar es Salaam katika Tamasha la wiki ya Mwananchi ambayo ni mahususi kutambulisha nyota wapya wa timu hiyo kabla ya msimu kuanza.