NI masaa tu kwa sasa yamebaki kabla ya dirisha la usajili kwa msimu wa 2021/22 kufungwa. Leo Agosti 31 milango iliyokuwa wazi inafungwa.
Sarakasi zimekuwa zikionekana kwenye timu zote kuhusu usajili hilo ni sawa. Ipo hivyo duniani kote hasa pale ambapo usajili unapofunguliwa ni asili ya mpira na mara nyingine bila hayo ule umakini unapungua kidogo.
Haina maana kwamba haya makosa yanapaswa kuwepo hapana ni mbaya kujirudia mara kwa mara kwa kuwa itafika wakati kunakuwa na muda mwingi wa kusikiliza kesi kuliko kufanya maendeleo kwa ajili ya timu zetu kusaka mafanikio.
Kwa namna soka letu la Bongo lilivyo nina amini kwamba zipo timu ambazo mpaka sasa hazijakamilisha usajili. Unaweza ukashangaa lakini huu ni ukweli na ipo wazi kabisa zipo timu wakati huu zinaanza kuingia sokoni kusaka wachezaji.
Viongozi wengine kwa sasa wanaanza kuwavutia waya wachezaji wao ili kujua kuhusu hatma yao kwa kuboresha mikataba yao. Kawaida na watakaoanza kumalizia leo nadhani watajipongeza kwamba wakikamilisha mpango kazi wao.
Kawaida kabisa pale usajili unapokaribia kufungwa wanaanza kuhangaika na wachezaji wapya na mtandao ukisumbua kidogo basi watasubiri huruma kutoka Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF) kuwaongezea muda.
Ukizunguka kote duniani ni soka la Bongo tupo kivyetuvyetu kuanzia staili ya uendeshaji na namna ya kumaliza mambo ambayo tunayafanya.
Wakati wenzetu wa Ulaya wakiwa wanaratiba yao kamili ya msimu mzima na kuanza mechi za ushindani hapa kwetu bado mambo hayajawa sawa kwa upande wa ratiba.
Pongezi kwa TFF kwa kuja na ile kalenda ya matukio tunaona kwamba wamekuwa tofauti kidogo kwa msimu huu basi inapaswa wawe tofauti katika kila jambo kwa msimu ujao kuanzia usimamizi mpaka umaliziaji wa yale ambayo wanayafanya.
Kwa wachezaji ambao wanaanza maisha mapya hao nina amini wanajua kile ambacho wanatakiwa kukifanya. Kuanza kwa ligi msimu wa 2021/22 kupo karibu na ni wakati mzuri kwa waliojiandaa na wakati mbaya kwa wale ambao bado hawajajiandaa.
Kazi ile ya kujua nani alisajiliwa kwa pendekezo la benchi la ufundi ama ilikuwa ni kwa pendekezo la kiongozi fulani inakuja pale ligi itakapoanza muhimu kujipanga kisaikolojia na kukubali matokeo yatakayotokea.
Pale watakapoanza kazi wanapaswa kufanya kazi kwa juhudi ili kuona kile wanachokihitaji kinatokea.
Juhudi isiyo kuwa ya kawaida katika kusaka matokeo pamoja na nidhamu ndani ya uwanja ni mambo ya kuzingatia. Muhimu ni kwamba hakuna ambaye anaweza kufikia malengo ikiwa hatakuwa na nidhamu.
Pia kwa TFF mbali na kuwekeza nguvu kubwa kwenye Ligi Kuu Bara basi kwa msimu ujao ni muhimu pia kuwekeza nguvu kubwa kwenye Ligi Daraja la Kwanza ambayo kwa sasa inaitwa Championship.
Endapo jicho kubwa litakuwa ndani ya ligi pekee na kuacha huku kwenye kiwanda cha kutengeneza timu shiriki bila kujali maisha yao itakuwa ni hatari kwa afya ya soka letu.
Ili soka liendelee ni lazima kuwe na misingi makini ambayo inaanzia huku chini na haijengwi kwa kubahatisha bali mipango makini na hesabu zenye uhakika.
Timu shiriki ndani ya Championship ni lazima zitambue namna gani zinaweza kufikia malengo yao hasa ukizingatia kwamba siku zinakwenda kasi na hazisubiri kwa yale makosa ambayo yalionekana msimu uliopita.
Njia ya kupata ushindi kwao ni moja tu kupambana na kufanyia kazi makosa yao ambayo waliyafanya kwenye mechi zao za mwanzo ikiwa walipata matokeo wana kazi ya kuendeleza rekodi ya kucheza bila kupoteza.