Home Makala KUUZWA KWA CHAMA NA LUIS..EDO KUMWEMBE AFUNGUKA HAYA..ASEMA SIMBA NI TIMU NDOGO

KUUZWA KWA CHAMA NA LUIS..EDO KUMWEMBE AFUNGUKA HAYA..ASEMA SIMBA NI TIMU NDOGO


BADO mashabiki wa Simba hawaamini kwamba mastaa wao, Luis Miquissone na Clatous Chama wameondoka. Chama ameonekana akiwa na jezi ya timu ya RS Berkane ya Morocco akiwa na swahiba wake mpya, Tuisila Kisinda. Mashabiki wa Simba wamegawanyika. Kuna fungu kubwa la mashabiki ambao wameulaumu uongozi wao kwa kuwauza Chama na Miquissone kwa pamoja. Hakuna anayelalamikia kuhusu madau yao. Wanalalamika kuhusu kuuzwa kwao kwa pamoja.

Hoja ya mashabiki ni kwamba uongozi umekosea kwa sababu timu ipo katika vita ya kuwania kutwaa ubingwa wa Afrika msimu ujao. Inashangaza kidogo, lakini mashabiki wa Simba wameanza kuamini timu yao inashindana na vigogo wengine kutwaa ubingwa wa Afrika.

Kitu ambacho mashabiki wanajisahaulisha ni kwamba Simba bado sio timu kubwa Afrika na kuwabakiza kina Chama kilikuwa kipimo cha ukubwa wao. Kivipi? Tumesikia kuna dau la dola 900,000 kwa Miquissone na kuna dau la dola 500,000 kwa Chama.

Viongozi wa Simba hawakupenda kuachana na mastaa hawa, lakini wamejikuta wamelazimishwa. Wakubwa wameweka mezani kiasi ambacho kinaonyesha ukubwa wao. Kama kweli Simba wangekuwa wakubwa kama mashabiki wao wanavyojiaminisha ni wazi viongozi wangekataa madau haya.

Lakini hapo hapo ukweli ni kwamba wachezaji hawa wanaenda kulipwa pesa ndefu. Kwa mfano, kama Chama alikuwa analipwa Shilingi 16 Milioni kwa mwezi akiwa Simba, Wamorocco wataenda kumlipa Shilingi 45 Milioni kwa mwezi.

Kama Miquissone alikuwa anachukua Shilingi 12 Milioni kwa mwezi pale Simba basi Al Ahly wataenda kumlipa Shilingi 34 Milioni kwa mwezi. Ili Simba wazigomee timu ambazo zinawataka mastaa hawa kwanza inabidi wafikie makubaliano ya mikataba mipya na mastaa hawa na waanze kuwalipa kile wangepata nje.

Kwa sasa Simba haina ubavu wa kutoa mishahara hiyo kwa kina Chama na hiki ni kipimo cha udogo wao katika soka la Afrika. mashabiki wengi wa Simba wanaangalia upande wa klabu yao tu bila ya kuangalia upande wa mishahara ambayo mastaa hao wanaenda kupata.

Samaki mkubwa anamla samaki mdogo ndivyo soka lilivyo. Simba ilikuwa imejichongea kufanya vizuri katika michuano ya Afrika. Nilijua tu kwamba wangekuwa wahanga wa mafanikio yao kwa sababu lazima kuna wachezaji ambao wangetakiwa na wakubwa. Bahati mbaya kwetu uchumi wa klabu unaifanya Simba kuwa timu mlishaji (feeder club) kwa wakubwa. Haijalishi mashabiki wana tamaa kiasi gani, lakini ukweli ni kwamba Simba na klabu nyingine nchini ziko chini kiuchumi kuweza kuwazuia wakubwa wasiwang’oe watu wao. Kama mashabiki wa Simba walitamani kuona timu yao ikianzia pale ilipoishia msimu uliopita ukweli ni kwamba hata mashabiki wa Ajax Amsterdam nao walikuwa wanatamani hivyo hivyo baada ya timu yao kufika nusu fainali ya Ulaya misimu michache iliyopita.

SOMA NA HII  MBALI NA CHICO USHINDI...HAWA HAPA MAPRO WENGINE WALIOSAJILIWA KWA MBWEMBWE NA KUISHIWA KUWA 'WATUMISHI HEWA'...

Nini kilifuata? Wakubwa walikwenda pale na kuwang’oa mastaa kina Matthijis de Ligt, Frenkie de Joing na wengineo. Hawakuwa na ubavu wa kuwazuia kutokana na dau kubwa ambalo liliwekwa katika meza yao. Leicester City walitwaa ubingwa wa England mwaka 2016 na mashabiki wao walipenda ndoto hiyo iendelee tena na tena. Nini kilifuata? Wakubwa waliwachukua kina Riyad Mahrez na N’Golo Kante. Maisha ni magumu kwa timu ambazo zina uchumi wa chini kulinganisha na wakubwa.

Ni kama ambavyo hapa nchini Simba na Yanga zina uwezo wa kuwang’oa wachezaji inaowataka katika klabu za Mtibwa Sugar, KMC, Mbeya City na nyinginezo. Basi na wao ndivyo ambavyo wamegeuzwa hivyo na wakubwa.

Usishangae kuona msimu ujao wakubwa wakarudi tena kumchukua Larry Bwalya au staa yeyote ambaye wataona anawafaa. Simba haina ubavu wa kuzuia hilo. Kitu cha kushukuru ni kwamba kwa sasa wachezaji wanauzwa kwa madau makubwa zaidi kuliko wakati ule waliouzwa Mbwana Samatta na Emmanuel Okwi. Labda kwa sababu thamani ya pesa imepanda maradufu.

Kitu cha msingi kwa Simba kwa sasa ni kuwa na jicho kali la kutafuta mastaa wengineo ambao watasababisha kikosi chao kiendelee kushindana kama ilivyokuwa msimu uliopita. Hata hivyo ukweli utabakia pale pale kwamba hata wakijitutumua kupata mastaa hao bado watageuzwa kuwa soko.

Makala haya yameandikwa na Edo Kumwembe na kuchapishwa kwenye gazeti la Mwanspoti.