Home news NDEMLA NDIO BASI TENA MSIMBAZI…ARUDISHWA BONGO KIMYA KIMYA…KUVAA UZI WA KIJANI AU…

NDEMLA NDIO BASI TENA MSIMBAZI…ARUDISHWA BONGO KIMYA KIMYA…KUVAA UZI WA KIJANI AU…


WAKATI mashabiki wa Simba wakisubiri kuona ni wachezaji gani wanaachwa katika kikosi chao kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu Bara na michuano ya kimataifa, tayari baadhi wametajwa kuanza kutafuta malisho kwingineko.

Ingawa dirisha la usajili la Ligi Kuu Bara bado lipo wazi, tayari Simba imekamilisha usajili wa nyota wake wapya, lakini haijatangaza wachezaji itakaowaacha.

Hata hivyo, baada ya kipindi kirefu wadau wa soka kutoa maoni yao wakimshauri kiungo mwenye mashuti makali ya mbali, Said Ndemla, kutazama kwingineko kutokana na kukosa namba katika kikosi cha kwanza cha mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara na Kombe la FA, msimu huu inaonekana wazi ameanza kutafuta malisho kwingine.

Ikumbukwe Ndemla ni miongoni mwa wachezaji walioongozana na kikosi cha Simba kwenda kuweka kambi ya kujiandaa na msimu mpya nchini Morocco, lakini amerejea nchini na tangu juzi yupo jijini Dar es Salaam.

Kaimu Ofisa Habari wa klabu hiyo, Ezekiel Kamwaga, alipoulizwa na mwandishi wetu kulikoni Ndemla amerejea nchini wakati si miongoni mwa wachezaji wanaounda kikosi cha timu ya Taifa, Taifa Stars, alisema ameomba udhuru na ana jambo lake binafsi.

“Ndemla ana ruhusa rasmi kutoka kwa uongozi wa Simba ndiyo maana aliondoka kambini, zaidi ya hapo hakuna kitu kingine ambacho kimefika mezani kwangu.

Hata hivyo, Ndemla anahusishwa kujiunga na KMC FC na Mtibwa Sugar inayovaa jezi za kijani na nyeupe, lakini alipoulizwa kuhusu tetesi hizo, Kamwaga alisema: “Sina taarifa hizo, tuwe wavumilivu taarifa zitatolewa rasmi na klabu kuhusu mchezaji gani anaondoka, yupi anaenda kwa mkopo na wangapi tumewasajili.”

Katibu Mkuu wa Klabu ya KMC, Walter Harson, kuhusu klabu hiyo kuwa katika mazungumzo ya kumsajili Ndemla, alisema hana uhakika kususu suala hilo na hajui kama kuna kiongozi kafanya naye mazungumzo.

“Naomba nipe muda nitakueleza kitu cha uhakika kwa sababu nilikuwa msibani na jioni hii (jana jioni) tutasafiri na timu kwenda kuweka kambi Morogoro, nikifika huko nitazungumza na makocha na viongozi wenzangu kisha nitakueleza,” alisema.

SOMA NA HII  USAJILI MPYA SIMBA WAMTISHIA AMANI KOCHA WA GEITA GOLD....AANZA KUOMBA 'POO' MAPEMA...

Mchezaji mwingine anayehusishwa na safari yake kuwadia kuondoka Simba ni beki wa kati, Ibrahim Ame, aliyejiunga na mabingwa hao msimu uliopita akitokea Coastal Union ya Tanga.

Ingawa Ame naye alikuwa na timu yake kambini Morocco, amerejea nchini na anadaiwa kufanya mazungumzo na Mtibwa Sugar na klabu yake inaelezwa ipo tayari kumtoa kwa mkopo.

Lakini Kamwaga alipoulizwa kuhusu Ame, alisema: “Ame naye aliomba ruhusu ana jambo lake, hivyo tusubiri kama kuna lolote nikiletewa mezani nitawajulisha.”

Alipoulizwa Msemaji wa Mtibwa Sugar, Thobias Kifaru, kuhusu klabu hiyo kufanya mazungumzo na Ame, alisema kuna wachezaji wengi wamezungumza nao ndani na nje ya nchi na kila kitu kitajulikana mwishoni mwa juma hili.

“Tupo kwenye mazungumzo na nyota kadhaa kuelekea msimu ujao, kwa sasa siwezi kutaja ila hadi mwisho wa juma tutahitimisha zoezi zima na kuwatangaza nyota wetu. Tanzania ni nchi kubwa na ina timu nyingi na hatufanyi mazungumzo na wa ndani tu hata wa kigeni pia, tupo kwenye mawindo tusubiri mwishoni mwa juma hili,” alisema Kifaru