Home Makala WAWAKILISHI WETU KIMATAIFA WAJIPANGE SAWASAWA

WAWAKILISHI WETU KIMATAIFA WAJIPANGE SAWASAWA


KILA Mtanzania kwa sasa anahitaji kuona timu zitakazopata nafasi kushiriki mashindano ya kimataifa zinajipanga sawasawa ili kuweza kufanya vizuri zaidi na zaidi.

Ni timu nne ambazo zitapeperusha bendera ya Tanzania kimataifa, katika Ligi ya Mabingwa tuna Simba na Yanga pia kwa upande wa Kombe la Shirikisho ni Azam FC na Biashara United.

Hapa tunakuletea namna ambavyo wawakilishi hao wanapaswa kujipanga kimataifa pamoja na mafanikio yao kwa msimu uliomeguka  wa 2020/21:-

Simba

Mabingwa mara nne mfululizo katika Ligi Kuu Tanzania Bara wamekuwa imara katika safu ya ushambuliaji. Kwa wakati  uliopo kwa sasa ikiwa ni hatua ya usajili jambo la msingi ni kuona namna gani kikosi kinaweza kuboreshwa kidogo na sio kubomolewa chote.

Imekuwa ikifanya vizuri kwenye safu ya ushambuliaji ambapo kwa misimu miwili ndani ya ligi imeweza kufunga mabao 156. Msimu wa 2019/20 ilitupia mabao 78 ambayo ni sawa na iliyotupia msimu wa 2020/21.

Safu yake ya ulinzi imekuwa ikiimarika taratibu ambapo kwa msimu wa 2019/20 baada ya kucheza jumla ya mechi 38 iliokota nyavuni mabao 21 ila kwa msimu wa 2020/21 imeokota nyavuni mabao 14.

 Katika misimu mitatu mfululizo imetoa wafungaji bora. Msimu wake wa 2018/19 mabao 23 msimu wa 2019/20 mabao 22 huyu ni Meddie Kagere na msimu wa 2020/21 alitupia mabao 13 na kwa msimu huu wa 2020/21 ni John Bocco alitupia mabao 16.

Mafanikio msimu 2020/21



 Mataji yote iliyosepa nayo msimu wa 2019/20 imeweza kuyatetea na sasa yapo kwenye mikono yao kwa mara nyingine tena. Walianza na Ngao ya Jamii kwa ushindi mbele ya Namungo, taji la ligi baada ya kukusanya pointi 83 na walimaliza na Kombe la Shirikisho kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya watani zao wa jadi, Yanga.

Ilifanikiwa pia kutinga hatua ya robo fainali katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

Yanga

Kikosi cha Yanga kinachonolewa na Kocha Mkuu, Nasreddine Nabi kimekuwa kikisuasua kwenye eneo la ushambuliaji hasa kwa safu yao kuwa na tatizo la ubutu licha ya kuwa ni namba mbili kwa kucheka na nyavu.

Ikiwa imetupia mabao 52 msimu huu mtupiaji wao namba moja ni Yacouba Songne alitupia mabao 8.

 Kwa washambuliaji wazawa ni pasua kichwa kwa kuwa Ditram Nchimbi ana bao moja, Wazir Junior ana mabao mawili hivyo ni kazi kwao kuongeza juhudi msimu ujao.

SOMA NA HII  ADAM SALAMBA: - NALIPWA MILIONI 161..AFUNGUKA JINSI ALIVYOJIUNGA NA TIMU YA MATAJIRI WA ALGERIA..ATAJA MADEM...

Mafanikio

Imeweza kumaliza ligi ikiwa nafasi ya pili na kuwa ni mshindi wa pili kwenye Kombe la Shirikisho. Kombe pekee ambalo wanalo kabatini kwa msimu huu ni lile la Mapinduzi na walisepa nalo kwa kushinda mbele ya Simba.


Kwa kuwa wanashiriki Ligi ya Mabingwa, wawakilishi hawa wa Tanzania ni lazima wajipange kufanya vizuri kimataifa.Maboresho iwe kwenye safu ya ushambuliaji pamoja na eneo la kiungo hasa mshambuliaji.

Azam FC

Wana kila kitu ambacho kinahitajika kwa timu kuwa nacho lakini hawajawa na mwendo mzuri hasa katika kusepa na mataji ambayo huwa wanayapigia hesabu. Taji lao moja tu la ligi ambalo walisepa nalo msimu wa 2003.


Wataipeperusha bendera ya Tanzania kimataifa katika Kombe la Shirikisho basi imani ya Watanzania ni kuona timu hii inafanya vizuri kila idara.


 Tayari Azam FC wameanza maboresho ya kikosi chao ambapo kuna baadhi ya nyota ikiwa ni pamoja na Obrey Chirwa, Ally Niyonzima, Yakub Mohamed na Mpiana Monzizi wamewekwa kando hivyo ambao watasajiliwa basi wakumbuke wana kazi ya kufanya kimataifa.


Mafanikio

Kumaliza ligi wakiwa nafasi ya tatu. Safu yao ya ushambuliaji imeweza kufunga mabao 50 ikiwa nafasi ya tatu. Uwepo wa Prince Dube umeweza kujibu ndani ya kikosi hicho akiwa ni namba moja kwa utupiaji na mabao yake ni 14 huku akiwa na pasi tano za mabao.


 Biashara United


Mlima mzito upo kwa wanajeshi wa Mpakani ambao inakuwa ni mara yao ya kwanza kushiriki mashindano ya kimataifa. Biashara United wasisahau kwamba ilikuwepo KMC wakati ule nafasi nne zilipotolewa kwa Tanzania kimataifa. KMC iliyumba kimataifa na iliporejea kwenye ligi haikuwa na mwendo mzuri.


Pia Namungo FC msimu uliopita ilipata ngekewa na kutinga hatua ya makundi ilikwama kukusanya hata pointi moja hivyo hii iwe darasa kwa Biashara United.


 Mafanikio

Kumaliza ligi ikiwa nafasi ya nne na kupata nafasi ya kushiriki Kombe la Shirikisho ni hatua kubwa kwao.

Maboresho makubwa yawe kwenye safu ya ushambuliaji kwa kuwa wamefanikiwa kufunga mabao 28 wakizidiwa na Gwambina FC ambayo imefunga jumla ya mabao 29 ila mwisho wa siku imeshuka daraja.