Home video YANGA: MOLOKO NI ZAIDI YA TUISILA KISINDA

YANGA: MOLOKO NI ZAIDI YA TUISILA KISINDA


 MAKAMU Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela, amemjaza upepo na kumpa sifa nyingi winga mpya wa timu hiyo, Mkongomani, Jesus Moloko akisema anaamini ataliziba pengo la Tuisila Kisinda.

Yanga imemsajili Moloko akitokea AS Vita ya DR Congo kwa ajili ya kuchukua nafasi ya Kisinda aliyeuzwa hivi karibuni kwenda RS Berkane ya nchini Morocco.


Akizungumza na Spoti Xtra, Mwakalebela alisema kuwa kati ya mawinga bora Congo, basi Moloko yupo, hivyo hawana hofu katika msimu ujao.



Mwakalebela alisema kuwa hawajakosea kumsajili winga huyo huku akiamini atatimiza majukumu ndani ya timu hiyo katika msimu ujao ambao wamepanga kubeba makombe yote watakayoshiriki.


“Hatujakosea kumsajili Moloko, kwani tukiwa kambini Morocco nimekuwa nikimfuatilia kwa karibu kwa ajili ya kujua uwezo wake.


“Kati ya usajili bora ambao tumeufanya katika msimu huu, basi huu wa Moloko ni mmoja wapo kutokana na kiwango kikubwa alichonacho.


“Kikubwa anachotakiwa ni kutimiza majukumu yake ya uwanjani kufunga na kutengeneza nafasi kwa wake ili timu ipate matokeo mazuri,” alisema Mwakalebela.


Kwa upande wa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga na Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM, Injinia Hersi Said ambaye alifanikisha usajili wa winga huyo, alisema:

 

“Kwa hakika Moloko ni mchezaji ‘potential’ ni mbadala sahihi wa Kisinda ambaye tumemuuza, kwangu namuona Moloko anakwenda kuwa mara tatu zaidi ya Kisinda kutokana na uwezo alionao.

 

“Jambo la kusubiri ni yeye afanye vizuri akiwa uwanjani, kwa sababu hilo ndiyo jambo la muhimu zaidi ambalo mashabiki wanatakiwa kumuombea,” .

SOMA NA HII  UTAPENDA ...WALICHOKIFANYA WACHEZAJI SIMBA WAKIWA MAZOEZINI..