MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Mohammed Dewji ‘MO’ amempa maagizo mazito kocha mkuu wa klabu hiyo Mfaransa, Didier Gomes kuhakikisha klabu hiyo inatwaa makombe yote ya ndani ambayo watashiriki na kufika angalau nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Msafara wa mwisho wa Simba uliokuwa nchini Morocco kwa ajili ya maandalizi ya kabla msimu ulirejea rasmi Jumapili, baada ya kipindi cha wiki tatu za maandalizi.
Katika kipindi hiko cha wiki tatu Simba walicheza michezo miwili ya kirafiki dhidi ya FAR Rabat na Olympique Club de Khouribga ambapo michezo yote iliisha kwa sare.
Kaimu Ofisa Habari wa Klabu ya Simba, Ezekiel Kamwaga alisema: “Baada ya kumaliza kambi yetu ya kwanza ya maandalizi ya kabla ya msimu ‘preseason’ kule Morocco na kikosi kurejea hapa nchini, sasa tunajipanga kuwa na kambi ya pili ya nje ya nchi ambayo tutaiweka wazi.
“Nikuhakikishie kuwa tumejizatiti kuhakikisha tunapiga hatua moja zaidi msimu ujao kulinganisha na msimu uliopita katika michuano yote tutakayoshiriki, tayari mwenyekiti wetu wa Bodi ya Wakurugenzi MO amekutana na kocha mkuu Didier Gomes na kumueleza matamanio yake ya kuhakikisha Simba inatwaa makombe yote ya ndani msimu ujao na kufika angalau nusu fainali ya Ligi ya mabingwa Afrika.”