MABEKI wazawa wawili ndani ya kikosi cha Simba, Shomari Kapombe ambaye ni ubavu wa kulia na Mohamed Hussein, ‘Tshabalala’ ambaye ni nahodha msaidizi wamekimbiza kwa kuyeyusha dakika nyingi ndani ya kikosi hicho kwa msimu wa 2020/21, jambo lililomkosha Kocha Mkuu, Didier Gomes.
Mbali na kukimbiza katika kuyeyusha dakika bado wazawa hao walikuwa ni mitambo ya kutengeneza mabao kwa kuwa walihusika katika jumla ya mabao 11 kati ya 78 ambapo Kapombe alitoa pasi sita za mabao na Tshabalala alifunga mabao mawili na pasi mbili za mabao.
Tshabalala alitumia jumla ya dakika 2,732 katika mechi 31 ambazo alicheza ndani ya ligi huku mshikaji wake Kapombe yeye akitumia jumla ya dakika 2,714 alicheza mechi 31.
Nyota hao wanatarajiwa kuendelelea pale walipoishia kwa msimu mpya wa 2021/22 kwa sababu bado wapo kwenye kikosi hicho kilichoweka kambi kwa muda nchini Morocco na sasa kimesharejea Dar.
Gomes aliliambia Championi Jumatatu kuwa anajivunia uwepo wa wachezaji wengi wenye uwezo mkubwa jambo ambalo linamfanya aamini kwamba watafanya vizuri kwenye mashindano ambayo watashiriki.
Simba inashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo msimu uliopita ilifanikiwa kutinga mpaka hatua ya robo fainali.
Ni nyota wake wawili itawakosa ambao ni Clatous Chama raia wa Zambia huyu yupo zake RS Berkane pamoja Luis Miquissone huyu yupo zake Al Ahly ya Misri na wote ni viungo.