BAADA ya kuondolewa Yanga Ofisa Mhamasishaji, Antonio Nugaz, uongozi wa klabu hiyo umefunguka kuwa mrithi wa nafasi hiyo atatangazwa hivi karibuni.
Yanga wamethibitisha kuachana na Nugaz katika nafasi ya Uhamasishaji baada ya dili lake la miaka miwili kuisha.
Kwa mujibu wa taarifa za ndani kutoka Yanga zinaeleza kuwa kilichomuondoa Nugaz ni mfumo wa mabadiliko unaoendelea ndani ya klabu, lakini pia kumalizika kwa mkataba.
“Kutokana na mchakato wa mfumo wa mabadiliko unaoendelea ndani ya klabu kwa sasa ndiyo uliopelekea kuondolewa kwa Nugaz ndani ya klabu hiyo kwa sasa.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela alifunguka kuwa Mtendaji Mkuu wa Yanga ndiye mwenye dhamana ya kupanga majukumu.
“Nugaz ameondolewa baada ya mkataba wake ambao ulikuwa wa miaka miwili kumalizika lakini pia kwa sasa tupo kwenye mchakato wa mabadiliko ya klabu hivyo kuna baadhi ya nafasi kwenye klabu zitaondolewa na zingine zitaongezeka.
“Hii inatokana na rasimu ya mabadiliko ya klabu ambayo ilipitishwa na wanachama kwenye mkutano mkuu wa klabu ambao ulifanyika hivi karibuni kuonyesha kila kitu ambacho kinapaswa kuwepo kwenye klabu.
“Kuhusu nafasi ya Haji Manara ndani ya klabu itajulikana hivi karibuni kwani mwenye dhamana ya kumpangia nafasi ni bosi wake ambaye ni Mtendaji Mkuu wa klabu (CEO), Senzo Mazingisa,” alisema Mwakalebela.