Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Ruvu Shooting Masau Bwire amewasihi Young Africans kuelekea mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika hatua ya awali dhidi ya Rivers United ya Nigeria.
Young Africans itaanzia nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam kesho Jumapili (Septemba 12), na kisha watakwenda Nigeria mwishoni mwa juma lijalo.
Masau ametoa nasaha kwa Young Africans kwa kuandika ujumbe mzito kwenye ukurasa wake wa Facebook.
Kesho, Jumapili, September 12, 2021, timu hii ya “Wananchi” itakuwa uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam ikiumana na timu kutoka nchini Nigeria katika kinyang’anyiro cha *Ligi ya Mabingwa* barani Afrika, hatua ya awali.
Ni mchezo muhimu, wenye uzito na umuhimu mkubwa kwa Young Africans kushinda na kujiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele zaidi.
Ushindi katika jambo lolote la ushindani ni mchakato, kujitoa na kujituma kwa wahusika (Wachezaji), pia, umoja, ushirikiano na mshikamano wa watu wote ni chagizo katika mafanikio na ushindi.
Vijana wetu, wachezaji wa Young Africans, watambue majukumu yao katika timu yao na mchezo huo wa Jumapili, wajue, mamilioni ya *Wananchi* tegemeo la ushindi katika mchezo huo ni wao, hivyo, wajitoe na kujituma sana, wacheze kwa moyo wote, wapambane kweli kweli, ushindi upatikane, hilo linawezekana!
Lakini pia, viongozi na uongozi wa Young Africans, unao wajibu mkubwa sana kuhakikisha ushindi katika mchezo huo unapatikana.
Viongozi wajitahidi kuwamotisha wachezaji, kuwatia moyo, kuwahamasisha na kuwajenga kisaikolojia, wawaaminishe wanaweza, na kweli waweze, ushindi upatikane.
Pamoja na mashabiki kuzuiwa kuingia uwanjani kutokana na changamoto ya maradhi ya Uviko 19, bado nafasi ya hamasa kwa wachezaji wenu ipo.
Kupitia matawi yenu, tumeni salaam na zawadi kwa wachezaji ili kuwamotisha na kujua kwamba mko nyuma yao, na kwamba hitaji, furaha na amani kwenu ni ushindi katika mchezo huo, watapambana, ushindi utapatikana.
Watanzania kwa ujumla wetu, bila kujali tofauti ya timu zetu, tuungane kwa pamoja, tuziombee mafanikio timu zetu nne, zinazoshiriki mashindano ya kimataifa ili ziweze kufanya vizuri.
Umoja ni nguvu, umoja ni mafanikio, tuungane Watanzania, tushikamane, tushirikiane, kwa pamoja kama taifa, tuzipambanie timu hizi, zifanye vema katika mashindano hayo, hii inawezekana na itakuwa imeliweka taifa letu katika mafanikio mapana kisoka, Afrika na Duniani kote!
Ambundo asisitiza kurejesha heshima Young Africans
Nitumie fursa hii, kuipongeza Biashara United, ambayo ikiwa ugenini imeweza kushinda mchezo wake wa awali. Tuwaombee pia Azam FC, waweze kuibuka na ushindi, iwe ushindi tu kwa timu zetu hizi zinazoshiriki mashindano hayo katika hatua ya awali!
Mungu ibariki Tanzania, zibariki timu zetu shiriki katika mashindano ya kimataifa.
Wananchi, *mbele daima*….
*Masau Kuliga Bwire – Mzalendo*.