WAKATI wengi wakiwa na hofu juu ya ujio wa Klabu ya TP Mazembe Tanzania kwa ajili ya mchezo wa kirafiki dhidi ya Simba, uongozi wa timu hiyo umethibitisha kwamba timu hiyo kutoka Congo inashuka Dar mapema.
TP Mazembe inatarajiwa kucheza na Simba, Septemba 19, Uwanja wa Mkapa kwenye mchezo wa kirafiki ikiwa ni siku ya tamasha la Simba Day ambalo kesho itakuwa ni Wiki la Simba linaanza.
Akizungumza na Spoti Xtra, Kaimu Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema kuwa mashabiki wasiwe na hofu TP Mazembe itawasili Dar na mchezo utachezwa bila mashaka.
“Kumekuwa na hofu juu ya ujio wa TP Mazembe lakini ninapenda kuwahakikishia mashabiki wa Simba kwamba timu hiyo inakuja na tunatarajia kuwapokea Septemba 18 kisha mchezo utakuwa Septemba 19.
“Hakuna sababu ya kuwa na mashaka juu ya hilo kwani wenyewe wamethibitisha hiyo tunaamini kwamba watakuja. Utaratibu mzuri wa kuwapokea utapangwa na mashabiki wataiona timu itakavyotua.
“Maandalizi kiujumla yanakwenda sawa kwani kuanzia zoezi la uuzaji wa tiketi kwa ajili ya Simba Day pamoja na namna ambavyo mashabiki walivyopanga kuwasili Uwanja wa Mkapa kwa wale ambao wanatoka nje ya Dar ulivyo ni mzuri na wameamua kuweka makutano kuwa Morogoro hivyo kuna mengi yanakuja,” alisema Kamwaga.