Home Makala HII HAPA A-Z STORI YA HANS POPE NA ISHU YA KUMPINDUA MWL...

HII HAPA A-Z STORI YA HANS POPE NA ISHU YA KUMPINDUA MWL NYERERE..RAIS MWINYI ALIHUSIKA


Wapenzi wengi wa mpira wa miguu, jumuiya ya wafanyabiashara na Watanzania kwa ujumla, usiku wa kuamkia jana walipatwa na huzuni kutokana na taarifa za kifo cha mfanyabiashara maarufu nchini, Zacharia Hans Poppe.

Ni huzuni inayotokana na ukweli kwamba alikuwa mwanamichezo wa kweli aliyependa michezo, hasa timu ya Simba aliyokuwa mwanachama na kiongozi.

Kwa wadau wa biashara, wamempoteza mtu aliyekuwa mhimili muhimu katika harakati zao.

Wiki iliyopita akizungumza na baadhi ya vyombo vya habari, Hans Poppe alikiri kuwa alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa Uviko –19, ambao usiku wa kuamkia jana ulikatisha safari ya maisha yake duniani.

Hadi mauti yanamfika katika Hospitali ya Aga Khan alikokuwa amelazwa kwa ajili ya matibabu, Hans Poppe alikuwa Mwenyekiti wa kamati ya usajili ya klabu ya Simba na mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa klabu hiyo.

Historia yake

Historia ya Hans Poppe inakwenda mbali zaidi ya ushiriki wake wa michezo. Aliwahi pia kuwa ofisa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na ni mmoja wa maofisa wa jeshi ambao walikamatwa mwaka 1983, wakituhumiwa kwa njama za uhaini wa kumpindua na kumuua Rais wa awamu ya kwanza, Mwalimu Julius Nyerere.

Hans Poppe alikuwa miongoni mwa zaidi ya Watanzania 32 waliokamatwa na miongoni mwa washtakiwa 19 waliofikishwa mahakamani na hatimaye kuhukumiwa. Katika kesi hiyo, Kapteni Zacharia alitetewa mahakamani na wakili aliyeitwa J. T. Tarimo na E. H. Mbuya.

Waliofikishwa mahakamani mwaka 1984, akiwamo Hans Poppe ni pamoja Luteni Kanali Martin Ngalomba, Kapteni Suleiman Metusela Kamando, Luteni Kanali Martin Peter Msami, Luteni Kanali Martin Ngalomba, Meja Reverian Bubelwa, Kapteni Vitalis Gabriel Mapunda na Kapteni Dietrich Oswald Mbogoro.

Wengine ni Kapteni Rodric Roshan Roberts, Kapteni Abdul Feshi Mketto, Kapteni Harry Hans Poppe, Kapteni Manyama Athumani Kazukamwe, Luteni Badru Rwechungura Kajaja, Luteni Pascal Christian Chaika na Luteni John Alphonce Chitungui.

Wengine ni Luteni Mark Augustine Mkude, Luteni John Simon Mbelwa Mzimba, Luteni Gervas B. Rweyongeza, Luteni Othar Thomas Haule, Luteni Nimrod Theophil Faraji na Luteni Michael Mwigulu.

Hans Pope na wenzake walisomewa maelezo ya awali ya mashtaka yao Ijumaa ya Novemba 23, 1984 mbele ya Jaji Anthony Bahati wa Mahakama Kuu, wakidaiwa kuwa katika kipindi cha Januari 10, 1983 kwa pamoja wakishirikiana na Pius Mutakubwa Lugangira au ‘Uncle Tom’ na Mohammed Mussa Tamim na watu wengine wasiofahamika walikula njama za kumuua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi ya Tanzania. Walidaiwa kuwa walikula njama kwa pamoja kutaka kuiangusha Serikali kati ya Juni 1982 na Januari 1983.

SOMA NA HII  USAJILI UMEKWISHA SASA KAZI NA INAANZA, TUSISAHAU LIGI YA WANAWAKE

Kesi hiyo, ambayo ni ya pili ya uhaini katika historia ya Tanzania Bara baada ya ile ya mwaka 1970, ilianza kutajwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu, Dar es Salaam, Ijumaa ya Januari 28, 1983, ikiwa ni karibu wiki moja tu baada ya Serikali kutoa taarifa kuwa ziligunduliwa njama za kutaka kuiangusha Serikali.

Hata hivyo, kesi hiyo ambayo awali ilikuwa ikiwakabili watu 30, ilifutwa Ijumaa ya Juni 17, 1983, ikiwa ni siku chache baada ya mshtakiwa wa kwanza, Pius Mutakubwa Lugangira au Uncle Tome au Father Tom na mshtakiwa wa pili, Hatty McGhee au Hatibu Gandhi, kutoroka wakiwa rumande na kusababisha washtakiwa wote wawekwe kizuizini.

Lakini kesi ilianza Jumatatu ya Septemba 17, 1984 ikiwa na washtakiwa 19. Baada ya kesi kusikilizwa Mahakama Kuu kwa karibu miezi saba, washtakiwa wanne, wote wakiwa wanajeshi wa JWTZ, walionekana hawana mashtaka ya kujibu na wakaachiwa huru Agosti 1985. Walioachiwa ni Luteni Mark Augustine Mkude, Luteni Gervas Rweyongeza, Luteni Paschal Chaika na Luteni Nimrod Theophil Faraji.

Ijumaa, Desemba 27, 1985 Jaji Kiongozi Nassor Mzavas aliyesikiliza kesi hiyo, katika hukumu yake alisema ni kweli kulikuwa na njama za kutaka kuiangusha Serikali kama ilivyodaiwa na upande wa mashtaka.

Alikuwa akimalizia kusoma hukumu yake aliyoianza tangu jana yake, Alhamisi ya Desemba 26, mbele ya washtakiwa wote, katika mahakama hiyo iliyojaa watu. Jaji Mzavas aliwahukumu washtakiwa vifungo vya maisha, lakini baada ya kutumikia vifungo vyao kwa miaka kumi, Hans Pope na wenzake waliachiwa huru kwa msamaha wa Rais wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, ikiwa ni mwezi mmoja kabla hajaondoka madarakani mwaka 1995.

Baadhi ya waandishi wa habari za michezo wanadai kuwa alipenda michezo tangu ujana wake na alianza kuipenda timu ya Simba mwanzoni kabisa mwa miaka ya 1970, akiwa kijana mdogo na kwamba mechi iliyomfanya atamke rasmi kuwa yeye ni Simba ilikuwa ni pale Simba walipocheza na watani wao, Yanga Jumamosi ya Juni 23, 1973, ambapo Simba ilishinda 1-0 kwa goli lililofungwa na Haidari Abeid ‘Muchacho’ katika dakika ya 68.