Home CAF KOCHA WA WASOMALI AKUBALI MUZIKI WA AZAM FC

KOCHA WA WASOMALI AKUBALI MUZIKI WA AZAM FC


 BAADA ya kushuhudia ubao wa Uwanja wa Azam Complex ukisoma Azam FC 3-1 Horseed FC kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho, Kocha Mkuu wa timu hiyo kutoka nchini Somalia amesema kuwa haikuwa bahati yao kuweza kushinda kwenye mchezo huo.

Katika mchezo huo kipindi cha kwanza timu zote mbili ziliweza kutupia bao mojamoja na yote yalisabishwa na mapigo huru ambapo kwa Horseed walioanza ilikuwa ni dakika ya 22 kupitia kwa Ibrahim Nor aliyepiga shuti lililomshida mlinda mlango Mathias Kigonya na Azam FC walijibu mapigo  kupitia kwa Ayoub Lyanga kwa kichwa akitumia mpira wa faulo uliopigwa na Idd Seleman, ‘Nado’.

Kocha Mkuu wa Horseed FC, Mohamed Hussein Ahmed amesema kuwa hawakuwa na cha kufanya kwa kuwa walizidiwa na wapinzani wao.

“Bahati mbaya sana kwetu tulizidiwa na wapinzani wetu kipindi cha pili lakini kipindi cha kwanza mambo yalikuwa sawa tulijitahidi. Azam FC ni timu nzuri hivyo kwa walichotuonyesha ni funzo kwetu ili tujipange zaidi kwa mchezo wetu ujao,” amesema.

Kwa upande wa Kocha Msaidizi wa Azam FC, Vivier Bahati amesema kuwa uwezo wa wachezaji pamoja na kambi ambayo waliifanya nchini Zambia ni moja ya sababu ya wao kuweza kushinda.

“Ukitazama mchezo ulikuwa mgumu na kila timu ilikuwa inahitaji ushindi, kwa kilichotokea ni pongezi kwa wachezaji kwani walifanya kile ambacho tuliwaambia. Kambi ya Zambia na maandalizi mazuri yametupa matokeo ila bado kazi inaendelea,” alisema.

Mchezo wa marudio unatarajiwa kuchezwa Septemba 18, Uwanja wa Uhuru ila wenyeji watakuwa ni Horseed FC kutoka Somalia.

SOMA NA HII  MASTAA YANGA WAIPIGA MKWARA MZITO ALAHLY