SUALA la usajili kwa sasa muda wake umekwisha na sasa macho na masikio ya mashabiki wengi ni kuelekea kuanza kwa msimu mpya wa 2021/22.
Zile purukushani za huyu katoka huku, yule kaingia pale zimekwisha na kwa sasa ni muda wa maandalizi umebaki tena unakwenda kasi sana kwa sababu siku hazisubiri na ratiba ishajulikana kwa kila timu.
Ukiwaweka kando hao wachezaji pia benchi la ufundi, viongozi nao tayari wameshaanza kupata picha ya kile ambacho wanakihitaji kwa ajili ya msimu ujao na nini mpaka sasa wanacho.
Hali hii inaleta picha nzuri kule ambako tunatarajia kwenda kutokana na kila mmoja kuwa na kitu ambacho anakifikiria kwa sasa na anakitenda kwa wakati.
Kila mmoja anajua kwamba msimu ujao hautakuwa na mchezomchezo tofauti na ule uliopita ambao nao ushindani wake haukuwa wa kitoto.
Hamna namna ya kufanya kwa sasa kwa kuwa maisha lazima yaendelee na kwa kuwa kwenye ushindani ni lazima uwepo ili ligi izidi kuwa bora zaidi. Lazima itatokea wapatikane wa kushuka na wale wa kupanda.
Zipo timu ambazo zilikuwa ndani ya ligi na sasa zinakwenda kuanza maisha mapya katika sehemu nyigine hilo lipo wazi na wanatakiwa waendelee kupambania kile ambacho wanakihitaji.
Kushindwa kwa sasa haina maana kwamba wao sio bora hapana ni hesabu tu zimewagomea wanaweza kujipanga upya wakarudi wakaendelea na kasi yao ile walipokuwa wanaanza msimu.
Hamna namna kila timu inapenda kupata matokeo mazuri ila picha kamili huwa inajengwa mwanzo hivyo kwa ajili ya msimu mpya mipango ianze mapema kabla ya mzunguko wa pili ambao ushindani wake huongezeka maradufu.
Kikubwa kinachohitajika ni maandalizi makini na kila mmoja kutimiza majukumu yake kwa wakati sahihi itaongeza ushindani na kuleta matokeo mazuri.
Ila imekuwa bahati mbaya kila wakati timu nyingi kuanza kuonyesha ushindani kwenye mzunguko wa pili ambao ni wa lala salama jambo ambalo linawaongezea ugumu kufanya vizuri.
Zile ambazo zinapanda kutoka Ligi Daraja la Kwanza ambayo kwa sasa inaitwa Championship zina kazi kubwa ya kuanza kufanya maandalizi ili ziweze kuleta ushindani wa kweli ndani ya ligi.
Kila kitu kinawezekana ikiwa kutakuwa na mpango makini na ukweli ni kwamba kupanda ni rahisi na kushuka ni rahisi pia lakini ukishashuka kurudi huku juu huwa inakuwa ngumu.
Stand United ilikuja ikashuka na ikashuka tena pale ilipokuwa kwenye Ligi Daraja la Kwanza. Singinda United ilikuja kwa kasi ila ghafla nayo kasi imekata na sasa hata Ligi Daraja la Kwanza nako imeshushwa.
Matukio haya yawe darasa kwa timu ambazo zinapambana kupanda kwenye ligi nazo zinapaswa zijue kwamba huku juu mambo sio mepesi kama ambavyo wanafikiria.
Matumaini yangu ni kwamba kupitia matukio haya yanayoendelea wamiliki wa timu, wachezaji pamoja na wamiliki wa timu wanaona namna mambo yanavyokwenda hivyo wataongeza umakini wakati watakapokuwa kwenye ushindani.
Tunataka kuona timu ikipanda kwenye ligi iwe na uwezo na vigezo vya kuhimili mikikimikiki ya huku kwani hakuna kuzubaa ni mwendo wa kukimbizana.
Ukiachana na ligi kuu ya wanaume pia kuna ligi ya wanawake hapa pia kuna umuhimu wa kuitazama kwa ukaribu ili kutengeneza timu makini pia kwa wanawake.
Kutokana na ushindani uliopo hasa kwenye timu za wanawake kuna umuhimu wa wadau kujitokeza pia kutoa sapoti kwa wanawake ili nao pia waweze kuleta ushindani.
Taratibu na kwenye ulimwengu wa soka la Wanawake nako kumeanza kuchangamka. Licha ya kwamba mabingwa Simba Queens wamekwama kufanya vizuri kimataifa ila wameanza kwa mwendo unaopendeza.
Iwe pia kwa mabingwa wajao pia kuweza kufanya vizuri zaidi na kupata matokeo chanya.