KOCHA Mkuu wa Simba, Mfaransa, Didier Gomes ni kama amewamaliza watani wake wa jadi, Yanga, ni baada ya kuzinasa video za michezo miwili waliyoicheza sawa na dakika 180.
Timu hizo zinatarajiwa kuvaana kesho Jumamosi saa 11:00 jioni katika mchezo wa Ngao ya Jamii utakaopigwa Uwanja wa Mkapa, Dar.
Katika mchezo huo, kila timu itaingia uwanjani ikiwa na mabadiliko ya kikosi chake baada ya kufanya usajili katika kuelekea msimu ujao kama ilivyo kwa Yanga ambapo kuna mshambuliaji wao tegemeo, Heritier Makambo.
Mmoja wa mabosi wa Simba kutoka ndani ya Benchi la Ufundi la timu hiyo, ameliambia Championi Jumatano, Gomes ameomba michezo miwili waliyoicheza wa Wiki ya Mwananchi waliyocheza dhidi ya Zanaco ya Zambia pamoja na ule wa kimataifa dhidi ya Rivers United uliochezwa kwenye Uwanja wa Mkapa.
Bosi huyo alisema kuwa, kocha anatarajiwa kukaa kikao na mtathmini viwango, Culvin Mavhunga kutoka nchini Zimbabwe ambaye alitoa mchango mkubwa kwa timu hiyo katika msimu uliopita.
Aliongeza kuwa mara baada ya kocha huyo kukaa kikao na Mzimbabwe, haraka atakutana na wachezaji wake jioni kwa ajili ya kuangalia video hizo na kikubwa kuangalia upungufu na uimara wa Yanga mpya.
“Kocha Gomes amekuwa na utaratibu wa kuangalia video za mechi za wapinzani walizozicheza kabla ya kukutana nao uwanjani.
“Tayari kocha ameagiza kupatiwa video mbili za michezo iliyopita ya Yanga ambayo ameicheza na aliyepewa kazi hiyo ni mtathmini viwango vya wachezaji ambaye ni Culvin.
“Tayari video hizo amezipata ambazo Yanga wamecheza dhidi ya Zanaco na Rivers na kikubwa anataka kuona ubora wa wapinzani kwa ajili ya kuangalia viwango vyao,” alisema bosi huyo.
Akizungumzia hilo, Kaimu Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema kuwa: “Hilo suala la benchi la ufundi na kingine nikizungumzia ninakua kama ninatoa siri za kambi, kikubwa timu inaendelea na maandalizi ya mchezo huo.”