PEP Guardiola,Kocha Mkuu wa Manchester City kwa sasa hana furaha kutokana na nyota wake wengi kusumbuliwa na majeraha huku ratiba yake ikiwa ni ngumu katika kusaka ushindi ndani ya Ligi Kuu England pamoja na Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Miongoni mwa nyota ambao hawapo sawa ni pamoja na John Stones ambaye anasumbuliwa na tatizo la misuli na Aymeric Laporte ambao kwa mujibu wa ripoti zinaeleza kuwa watakuwa nje ya uwanja kwa muda wa wiki mbili hivyo katika hali halisi watakosa mechi zote tatu na wote ni mabeki.
Mechi hizo ambazo watakosa ni pamoja na ile dhidi ya Chelsea, kesho Septemba 25 ambao ni wa ligi pia ana kazi ya kukutana na Lionel Messi na Neymar wanaokipiga ndani ya PSG, Septemba 28 katika mchezo wa UEFA Champions League kisha Oktoba 3 ana kazi mbele ya Liverpool katika mchezo wa ligi bila uwepo wa nyota wake hao ambao ni tegemeo katika kikosi cha City.
Mabingwa hao watetezi City wanakutana na Chelsea ambayo imewaka ikiwa na Romelu Lukaku chini ya Kocha Mkuu, Thomas Tuchel ambapo ipo nafasi ya kwanza na pointi 13 huku City ikiwa nafasi ya tano na pointi 10 zote zimecheza mechi tano jambo ambalo linampasua kichwa Guardiola.
Kwa sasa Guardiola yupo kwenye mtihani mzito ambapo ameamua kuwatumia vijana wa City katika mechi zake ili kuweza kuwapa nafasi ya kusaka ushindi kwenye mechi za ushindani huku akisifu uwezo wa vijana hao.