Home news IFAHAMU SABABU ZA SHOMARI KAPOMBE KUWA NAHODHA WA SIMBA

IFAHAMU SABABU ZA SHOMARI KAPOMBE KUWA NAHODHA WA SIMBA


 HIVI unajua kisa cha Kocha wa Simba, Didier Gomes kumvua kitambaa cha unahodha msaidizi Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ na kukihamisha kitambaa kwa Shomari Kapombe? Championi linakupa jibu.

Kama hujui hilo basi tambua kwamba kisa hicho kimetoka baada ya mwenendo wa kiwango bora cha uchezaji wa Kapombe ambacho kimekuwa kivutio kikubwa kwa kocha Gomes na kusababisha ampe uongozi ndani ya timu.

Hata hivyo, Tshabalala atabaki kuwa nahodha namba tatu wakati Kapombe ni namba mbili na John Bocco akiwa namba moja.

Kwenye mchezo wa TP Mazembe na Simba, uliopigwa Jumapili iliyopita huku wakibamizwa kwa bao 1-0, siku hiyo Kapombe alitinga uwanjani akiwa ametinga kitambaa cha unahodha huku Tshabalala akiwa uwanjani.


Chanzo chetu cha ndani kutoka kambi ya Simba iliyokuwa Karatu, Arusha, kimeweka bayana kwamba, Gomes amekuwa akivutiwa zaidi na nidhamu na uwezo wa Kapombe jambo lililomfanya kumpandisha kutoka nafasi ya nahodha namba tatu na kumfanya awe msaidizi wa Bocco.

“Watu wengi wanajiuliza sana suala la Kapombe kuvaa kitambaa cha unahodha dhidi ya TP Mazembe, ila majibu ya wazi yako hivi, Gomes ndiye mwenye jukumu la kuchagua nahodha anayemtaka kwani nafasi ya nahodha uwanjani huwa ni muhimu sana kwa kocha kwani yeye ndiye humsaidia kufikisha taarifa zote wakati wa mechi.

“Hivyo tangu alipoanza kukinoa kikosi chetu amekuwa muumini zaidi wa hilo na ndiyo maana utaona ameamua kumpandisha Kapombe kuwa nahodha msaidizi kutokana na ushawishi alionao kwa wachezaji wenzake,” kilisema chanzo hicho.

Alipotafutwa Mratibu wa Simba, Abbas Ally azungumzie ishu hiyo alisema: “Kocha wetu tangu alipokabidhiwa timu amekuwa akiteua nahodha msaidizi kutokana na uwezo wake kwenye mazoezi, hivyo Kapombe alipewa nafasi hiyo baada ya kuonyesha juhudi kubwa lakini hata nidhamu yake imetosha sana kwa kocha kujiridhisha hadi kumpatia kitambaa cha nahodha msaidizi.”


SOMA NA HII  ALLY KAMWE AJITWIKA ZIGO LA ZILIPO BILIONI 1.5 ZA JEZI....AFUNGUKA MIL 300 ILIYOSEMWA NA INJINIA HERSI...