SEPTEMBA 25, mwaka huu moto utawaka tena katika Uwanja wa Mkapa ambapo Watani wa Jadi, Simba na Yanga watashuka kuumana kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii ambao ni maalum kwa ajili ya ufunguzi wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2021/22.
Yanga wataingia kwenye mchezo huu wakiwa na kumbukumbu ya kupoteza dhidi ya Simba kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii uliopigwa Agosti 23, mwaka 2017 ambapo Simba walifanikiwa kutwaa taji hili baada ya kuibuka na ushindi wa mikwaju ya penalti 5-4.
Wakati pambano hili likisubiriwa kwa hamu na mashabiki wa timu hizi kongwe nchini, kuna shughuli pevu itakuwa katikati ya uwanja ambapo kutakuwa na bato la nyota wa vikosi vyote viwili ambao watakuwa wakionyeshana umwamba wao.
Championi Jumatano linakuletea baadhi ya wachezaji wa Simba na Yanga ambao bato lao ndani ya dakika tisini litakuwa si la kitoto.
HERITIER MAKAMBO V JOASH ONYANGO
Msimu uliopita tulishuhudia bato kali kati ya beki kisiki wa Simba, Joash Onyango na aliyekuwa winga wa Yanga, Tuisila Kisinda kwenye mchezo wa raundi ya kwanza Onyango alimchezea madhambi Kisinda kutokana na kushindwa kuendana na spidi ya winga huyo jambo ambalo liliwapa faida Wananchi wakapata mkwaju wa penalti.
Baada ya Kisinda kuondoka msimu huu Yanga wamefanikiwa kumrudisha straika wao Heritier Makambo ambaye ni miongoni mwa mastraika hatari kwa kucheka na nyavu. Katika mchezo wa Jumamosi mashabiki wengi wanasubiri kuona kati ya Onyango na Makambo ni nani atamtambia mwenzake.
SADIO KANOUTE V YANNICK BANGALA
Wote hawa wanaonja ladha ya mechi ya watani kwa mara ya kwanza. Sadio Kanoute amejiunga na Simba msimu huu akitokea Klabu ya Stade Malien ya Mali huku Bangala ambaye amewahi kukipiga AS Vita amesaini kandarasi ya miaka miwili kukitumikia kikosi cha mabingwa mara 27 wa ligi.
Kanoute na Bangala wote wana sifa ya utulivu na ni wazuri kwenye kuzuia hivyo bato lao kwenye eneo la kiungo linatarajiwa kuwa la kibabe.
TADDEO LWANGA V KHALID AUCHO
Vita nyingine ambayo inasubiriwa kwa hamu kubwa kwenye mchezo huu ni kati ya viungo wa timu ya taifa ya Uganda Khalid Aucho wa Yanga na Taddeo Lwanga wa Simba.
Katika nusu msimu ambao Lwanga aliitumikia Simba kwa kiasi kikubwa alifanikiwa kuonyesha kiwango bora akihudumu kwenye eneo la kiungo mkabaji. Jumamosi hii Lwanga atakutana uso kwa uso na Aucho kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii ambapo vita ya Waganda hawa itakuwa siyo ya kitoto.
DJUMA SHABANI V PETER BANDA
Djuma Shabani atakuwa na kibarua kigumu kuhakikisha anamzuia kiungo fundi wa Simba, Mmalawi Peter Banda ambaye kwenye mchezo dhidi ya TP Mazembe alionyesha kiwango bora licha ya kucheza dakika chache.
OUSMANE SAKHO V FEISAL
Kwenye eneo la kiungo cha juu kuna vita nyingine ambayo inasubiriwa kwa hamu kwenye mchezo huu ambapo mafundi wawili wataonyeshana umwamba. Feisal Salum wa Yanga na Ousmane Sakho ambao wote hawa ni mafundi kwelikweli.
Sakho ni ingizo jipya kwenye kikosi cha Simba akitokea Tengueth FC ya kwao Senegal ambapo hadi sasa ameonyesha kiwango bora ndani ya kikosi cha Simba akifunga mabao matatu kwenye mechi tano za kirafiki alizocheza.
JESUS MOLOKO V MOHAMMED HUSSEIN ‘ZIMBWE JR’
Msimu uliopita tulishuhudia vita kubwa kati ya Tuisila Kisinda wa Yanga na Mohammed Hussein ‘Zimbwe Jr’ wa Simba kwenye mechi za Watani wa Jadi.
Zimbwe ndiye mchezaji pekee aliyefanikiwa kumdhibiti Kisinda kwenye kila mechi ambayo Simba na Yanga zilikutana licha ya spidi ya winga huyo ambaye kwa sasa anakipiga RS Berkane. Msimu huu Zimbwe ana kibarua kingine dhidi ya winga mpya wa Yanga Jesus Moloko ambaye anasifika kwa kucheza soka la kasi.
WENGINE HAWA HAPA
Duncan Nyoni Vs Adeyum Saleh Kibu Dennis Vs Bakari Mwamnyeto Fiston Mayele Vs Pascal Wawa.