Home news ZAWADI YA MAYELE KUTOKA SIMBA, MASHABIKI KUMBE WALISUSA

ZAWADI YA MAYELE KUTOKA SIMBA, MASHABIKI KUMBE WALISUSA


TAYARI ngoma ipo uwanjani na leo Ligi Kuu Bara inatarajiwa kuanza kwa timu mbalimbali kusaka ushindi.

Ikumbukwe kwamba Septemba 25 ulichezwa mchezo wa Ngao ya Jamii na ni Yanga inayonolewa na Kocha Mkuu, Nasreddine Nabi ilisepa na ushindi wa bao 1-0 mbele ya Simba inayonolewa na Kocha Mkuu, Didier Gomes.

Hapa Championi Jumatatu inakuletea mambo 8 ambayo yalibamba kwenye mchezo huo wa kukata na mundu:-

Watoto na Nembo za timu

Kabla ya mchezo wa Ngao ya Jamii kuanza nembo za timu zote ambazo zitashiriki Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2021/22 ziliweza kuonyeshwa kwa mashabiki wote waliojitokeza pamoja na wale ambao walikuwa wanatazama Azam TV.

Watoto hao walikuwa ni moja ya sehemu ambayo ilivuta hisia za mashabiki wengi kwa kuwa ilikuwa ni katika mpangilio mzuri na muonekano wao ulikuwa ni wa kuvutia kwa timu zote 16.

Manara na shangwe

Haji Manara, Ofisa Habari wa Yanga aliweza kuibua shangwe mwanzo mwisho baada ya kuingia Uwanja wa Mkapa na kuketi eneo la mashabiki wa Yanga kuongeza nguvu kwenye ushangiliaji.

Baada ya Yanga kushinda kwa bao 1-0 mbele ya Simba aliweza kushuka na kuzunguka uwanja huku akiwa ametoa jezi yake na aliigawa kwa mashabiki.


Kaze naye ana watu

Kabla ya mchezo kuanza Cedric Kaze ambaye ni Kocha Msaidizi wa Yanga aliweza kuibuka katika Uwanja wa Mkapa ambapo mashabiki walipomuona waliibua shangwe kama lote kumshangilia kocha huyo.

Kaze anarejea tena ndani ya Yanga baada ya kufanya kazi hapo msimu uliopita wa 2020/21 kabla ya kuchimbishwa kazi kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni mwendo mbovu wa timu hiyo ila kwa sasa amerejeshwa tena kuendeleza gurudumu na bosi wake ni Nasreddine Nabi.

Mashabiki wa Simba walisusa

Haikuwa dabi yenye mashabiki wengi hasa kwa upande wa Simba huenda ni jambo lililowatoa mchezoni Simba kwa kuwa hawajazoea kucheza bila kuwa na mashabiki wengi.

Pia amshaamsha zilikuwa za kishkaji sana kwenye mchezo huo Uwanja wa Mkapa jambo ambalo liliwapa nguvu Yanga na ilionyesha kuwa mashabiki wa Simba waliisusia mechi hiyo.

SOMA NA HII  WAKATI CHAMA NA PHIRI WAKIPEWA SIFA...MGUNDA AIBUKA NA KUANIKA HILI KUHUSU KUIFUNGA COASTAL JUZI....

Mayele apewa zawadi na Simba

Baada ya Fiston Mayele kumaliza kazi ya kumtungua Aishi Manula kwa shuti kali na kuanza kushangilia walipo mashabiki wa Simba alipewa zawadi yake ya kutupiwa chupa na mashabiki wa Simba waliopoteza tabasamu mapema kabisa.

Mayele alionekana kutojali kwa kuwa aliendelea kushangilia mpaka muda aliorejea uwanjani kuendelea kuitumikia timu yake hiyo.

Shujaa Mauya benchi Lwanga ndani

Mashujaa wa mwisho kufunga kwenye mechi zao za karibuni ilikuwa ni viungo ambapo kwa Simba kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho alikuwa ni Taddeo Lwanga aliyepachika bao hilo huko Kigoma.

Kwa upande wa Yanga shujaa wao alikuwa ni Zawad Mauya. Mashabiki wengi walitarajia nyota wote wataanza kikosi cha kwanza ila mambo yalikuwa tofauti.

Mauya kwa Yanga yeye alianzia benchi huku Lwanga kwa Simba yeye alianza kikosi cha kwanza na alikwama kuyeyusha dakika zote 90 kwa kuwa alionyeshwa kadi nyekundu baada ya kuonyeshwa kadi mbili za njano.

Wawa baba lao

Katika mchezo huo ni Pascal Wawa alikuwa ni baba lao kwa kuwa alikuwa ni mchezaji pekee aliyebarikiwa kuwa na miaka mingi ambayo ni 35 na alipiga kazi kwelikweli licha ya timu yake ya Simba kufungwa.

Katika eneo la ulinzi mwamba huyu alibaki kuwa kiongozi baada ya mshikaji wake Joash Onyango mwenye miaka 28 kuweza kuumia kwenye mchezo huo jambo lililofanya ngome ya ulinzi iwe miguuni mwa Wawa.

Aliweza kuokoa hatari 10 zilizokuwa zinamfuata Aishi Manula na mipira yake ile mirefu ilikua inafika eneo husika ila tatizo huko ilikokuwa inakwenda ilikuwa inakutana na balaa la washkaji makatili waliokuwa wanaongozwa na Bakari Mwamnyeto wa Yanga.

Benchi la Simba mnuno kama wote

Unaambiwa hakuna aliyetabasamu wakati wa kutoka kwa benchi la ufundi la Simba likiongozwa na Gomes baada ya kupoteza mchezo huo wa Ngao ya Jamii, ulitembezwa mnuno wa maana huku wachezaji nao wakiwa hawana furaha ya kupoteza taji walilokuwa wanatetea.

Kwa upande wa Yanga ilikuwa ni furaha kama yote kwa kuwa walikuwa wamesepa na taji hilo mbele ya watani zao wa jadi.