NI mwendo wa mashuti tu! Ndivyo unaweza kusema kutokana na namna mazoezi ya Simba leo jioni yalivyokuwa kwenye Uwanja wa Karume, Musoma ikijiandaa na mechi ya leo dhidi ya wenyeji Biashara United.
Simba ilianza mazoezi hayo Saa 10:40 jioni kwa wachezaji kunyoosha viungo kwa kukimbia kidogo na kuruka koni kisha wakaenda katika programu nyingine.
Wachezaji hao walikuwa 23, ambao ni makipa watatu Aishi Manula, Beno Kakolanya, na Ally Salim, mabeki Shomari Kapombe, Mohamed Hussein, Israel Mwenda, Kennedy Juma, Erasto Nyoni, Henoc Inonga na Pascal Wawa.
Viungo ni Thadeo Lwanga, Muzamiru Yassin, Peter Banda, Rally Bwalya, Pape Sakho, Jimmyson Mwanuke, Yusuph Mhilu, Duncan Nyoni na Hassan Dilunga.
Washambuliaji ni John Bocco, Meddie Kagere, Chris Mugalu, na Kibu Denis.
Baada ya kunyoosha misuli walienda katikati ya Uwanja na kuanza kucheza zubaisha bwege kama kwa muda wa dakika 15 hivi kisha kuhamia kwenye mbinu za kufunga.
Erasto Nyoni, Kapombe, kennedy, Israel, Wawa, Tshabalala na Lwanga hawakuwa sehemu ya mazoezi hayo ya kufunga walibaki katikati ya Uwanja na kupiga stori mbili tatu.
Wengine wote walienda katika moja ya goli la Uwanja huu na kuanza kuelekezwa na kocha mkuu, Didier Gomes na msaidizi Seleman Matola.
Hapo wachezaji wengine walikuwa wakipigiana pasi zisizoziti tatu na kuzipenyeza katika eneo la boksi la 18 ambapo ziliwakuta Kibu, Bocco na Kagere ambao walimfunga mara kwa mara kipa Aishi Manula mabao yasiyopungua matano kwa kila mmoja.
Muda huo Gomes alikua akiwasisitiza kupiga mashuti yenye uzito na walifanya hivyo na kuonekana kumkosha.
Mugalu ambaye ni mshambuliaji pia hakuhusika katika programu hiyo kwani baada ya kunyoosha viungo alitoka na kwenda kukaa jukwaa la viongozi.
Saa 11:40 kocha Gomes alifunga rasmi mazoezi hayo na kuongea mawili matatu kisha kuondoka uwanjani hapo kwa gari ndogo aina ya Coasta kurejea kambini kwao kwenye hotel ya Matvila.