Home news SABABU ZA KAZE KURUDI YANGA HIZI HAPA

SABABU ZA KAZE KURUDI YANGA HIZI HAPA


CEDRICK Kaze, anatarajiwa kutambulishwa muda wowote kwa mashabiki wa Yanga baada ya kutua kimyakimya usiku wa kuamkia jana, Septemba 23.

Kaze anatajwa kurejea ndani ya timu hiyo kuja kuwa msaidizi wa kocha wa sasa Nasrredine Mohamed Nabi ambaye kwa muda sasa amekuwa akifanya kazi peke yake.

Kaze aliondoka ndani ya timu hiyo mwishoni mwa msimu uliopita kufuatia mwendelezo wa matokeo yasiyoridhisha ambayo Yanga walikuwa wanavuna kwenye Ligi Kuu Bara.

Mmoja wa viongozi wa juu wa Yanga, ameliambia Championi Jumatano kuwa, zipo sababu za Kaze kurejeshwa Yanga ambazo ni elimu, uzoefu wa soka la Bongo na lugha.

“Leseni yake ya ukocha (leseni A ya CAF), ni sababu kubwa ya Kaze kurejeshwa Yanga. Viongozi wanaona hii itawasaidia Yanga kuwa chini ya makocha ambao wana leseni kubwa kutoka kwenye Shirikisho la Soka Afrika.

“Jambo lingine ni lugha, Kaze ni mzuri sana kwenye kuzungumza lugha nne kwa ufasaha ambazo ni Kiswahili, Kiingereza, Kifaransa na Kirundi, ndani ya timu kuna wachezaji wenye kutumia hizo lugha zote nne.

“Hivyo itakuwa rahisi kwa Kaze kuweka daraja kati ya kocha mkuu na wachezaji, pia itapunguza gharama za kuwa na mkalimani wa timu.

“Lakini Kaze ni mzuri kwenye mbinu na mikakati, ni rahisi kwa kocha mkuu kubadilisha mbinu na mipango ya timu, programu za mazoezi punde tu anapopewa ushauri na msaidizi wake ambaye naye ni kocha mzuri.

“Kaze ameishi Tanzania akiifundisha Yanga kwa takriban miezi sita, anavijua vizuri viwanja vya mikoani, hivyo ni rahisi kumsaidia mwalimu juu ya uchaguzi wa wachezaji sahihi kwenye viwanja tofauti.”


Mkurugenzi wa Mashindano wa Yanga, Thabit Kandoro, aliliambia Championi Jumatano kuwa, wapo kwenye mchakato wa kutafuta kocha msaidizi kwa sasa ingawa siyo kweli wamemalizana na Kaze kwa sababu bodi haijakaa na kujadili suala hilo.


SOMA NA HII  BAADA YA SOKA LA KIBABE JANA....HII HAPA RATIBA NZIMA YA MPAPATUKO WA LIGI KUU YA NBC KWA LEO...USIKOSE....