Home Makala WAMESEPA ILA WAMEACHA ALAMA KUELEKEA KARIAKOO DABI

WAMESEPA ILA WAMEACHA ALAMA KUELEKEA KARIAKOO DABI


 KINAWASHWA tena Jumamosi hii pale kwa Mkapa, ndiyo pazia la Ligi Kuu Bara litafunguliwa rasmi siku hiyo ya Septemba 25, kwa mchezo mkali wa Ngao ya Jamii utakaozikutanisha klabu watani wa jadi kutoka Kariakoo Simba dhidi ya Yanga.


Mchezo huu ambao kwa kawaida huvuta hisia za mashabiki wengi wa kabumbu ndani na nje ya mipaka ya Tanzania, unasubiriwa kwa hamu hasa kutokana na mabadiliko makubwa ambayo vikosi hivi vimeyafanya kupitia dirisha la usajili lililofungwa Agosti 31, mwaka huu.

Kuelekea mchezo huo mkubwa, wapo baadhi ya nyota wa kimataifa ambao walikuwa hawakosekani kwenye Kariakoo Dabi kutokana na ubora wao, lakini kwa sasa tayari wamezihama timu hizo. Championi Jumatano linakuletea listi ya mastaa ambao waeondoka na kuacha rekodi kubwa kwenye Kariakoo Dabi. 


CLATOUS CHAMA


Baada ya utumishi wake wa misimu mitatu ndani ya kikosi cha mabingwa watetezi wa ligi kuu, Simba, hatimaye mashabiki wa klabu hiyo na wadau wa soka nchini wataushuhudia msimu mpya bila uwepo wa aliyekuwa kiungo fundi wa Mzambia, Clatous Chama ambaye amejiunga na RS Berkane ya Morocco.

Chama alikuwa miongoni mwa nyota ambao wamekuwa wakinogesha sana mchezo wa dabi kutokana na ufundi wake wa kufunga na kutengeneza nafasi za kufunga mabao, Chama alihusika moja kwa moja kuimaliza Yanga kwenye nusu fainali ya FA, Julai 12, mwaka jana ambapo Simba walishinda mabao 4-1.

Msimu uliopita akiwa na Simba, Chama kwenye ligi Kuu alicheza michezo 28 na kuhusika kwenye mabao 23 akifunga mabao nane na kuasisti mara 15.


FAROUKH SHIKALO


Msimu ujao anatarajiwa kuuwasha moto ndani ya kikosi cha KMC, baada ya kukamilisha usajili wake kama mchezaji huru kufuatia kumaliza mkataba wake Yanga.

Licha ya mapungufu aliyokuwa nayo, Shikalo anatajwa kuwa miongoni mwa makipa bora wa kigeni ambao wamecheza msimu uliopita. Katika kuthibitisha hilo, Shikalo akiwa na Yanga aliwahi kusimama langoni kwenye michezo minne ya dabi ya Kariakoo dhidi ya Simba ambapo aliruhusu kufungwa mchezo mmoja tu wa fainali ya FA wa Julai 25, mwaka huu. 


Michezo miwili iliisha kwa sare ikiwemo mchezo wa fainali ya Kombe la Mapinduzi Januari 13, mwaka huu ambapo Yanga waliibuka mabingwa na ule wa Januari 4, mwaka jana ukiisha sare ya 2-2, huku Julai 3, mwaka huu akiiongoza Yanga kuifunga Simba bao 1-0.


 


LUIS MIQUISSONE


Huyu ni miongoni mwa wachezaji bora zaidi ambao wamepita ndani ya kikosi cha Simba katika miaka ya hivi karibuni, ambapo alihudumu ndani ya kikosi hicho kwa kipindi cha msimu mmoja na nusu.

Akiwa na Simba, Luis aliunda pacha hatari na kiungo Mzambia, Chama ambapo kwa pamoja msimu uliopita kwenye ligi kuu pekee walihusika kwenye mabao 56, walifunga mabao 25 na kuasisti mara 31.

SOMA NA HII  MZIKI MZIMA WA SIMBA NA YANGA HUU HAPA


 


Luis pia alikuwa mchezaji hatari linapokuja suala la dabi, ambapo katika michezo hiyo alifanikiwa kuhusika kwenye mabao matatu, alifunga bao moja dhidi ya Yanga kwenye ushindi wa mabao 4-1 mchezo wa nusu fainali ya FA Julai 12, mwaka jana, na kutoa asisti mbili moja ikiwa ni kwenye sare ya bao 1-1 Novemba 7, mwaka jana na ishindi wa 1-0 Julai 25, mwaka huu.

MICHAEL SARPONG

Alianza kwa mkwara mkubwa kwenye ardhi ya Tanzania akifanikiwa kufunga katika michezo miwili mfululizo ya kwanza. Sarpong alianza makeke yake kwa kuwatungua vigogo wa Burundi, klabu ya Aigle Noir kwa bao la dakika ya 59 katika ushindi wa mabao 2-0 walioupata Yanga katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki Agosti 30, mwaka jana.


Sarpong akafunga tena katika mchezo wa ufunguzi wa msimu uliopita pale Yanga walipopata sare ya bao 1-1 dhidi ya Prisons. 


Licha ya kutokuwa na msimu mzuri akiwa na Yanga, lakini Sarpong ameacha alama ya kubwa kwa kufunga bao katika mchezo wa Dabi ya Kariakoo akifanya hivyo Novemba 7, mwaka jana katika mchezo wa mzunguko wa kwanza ulioisha kwa sare ya bao 1-1.


TUISILA KISINDA


Uhamisho wake wa kujiunga na vigogo wa Morocco RS Berkane akitokea Yanga, inawezekana ukawa ni miongoni mwa mambo yaliyowafurahisha zaidi mabeki waliokuwa wakicheza dhidi ya Yanga, hii ni kutokana na mateso makubwa aliyokuwa akiwapatia kutokana na kuwa na kasi kubwa uwanjani.


Kisinda aliyeichezea Yanga kwa kipindi cha msimu mmoja uliopita na kuhusika kwenye mabao 12, naye alikuwa mwiba mkali kwa mabeki wa Simba hasa katika michezo ya Dabi ya Kariakoo. Atakumbukwa sana na Wanayanga kupitia penalti aliyoitengeneza Novemba 7, mwaka jana baada ya kumlambisha nyasi mlinzi wa kati wa Simba, Joash Onyango.

LAMINE MORO


Kitasa wa kimataifa wa Ghana ambaye alihudumu kwa mafanikio makubwa ndani ya Yanga kwa kipindi cha misimu miwili kabla ya kutupiwa virago mwishoni mwa msimu uliopita wa 2021, ambapo anatajwa kujiunga na Rayon Sports ya Rwanda.


 


Achana na stori zake za nje ya uwanja, Lamine ni beki haswa na ambaye alikuwa na mchango mkubwa kwenye kikosi cha Yanga awapo uwanjani hasa anapokuwa hana majeraha.


Msimu uliopita alikuwa miongoni mwa mabeki waliofunga mabao mengi zaidi ambapo alitupia manne kwenye ligi kuu.

Alikuwa mchezaji imara kwenye Dabi ya Kariakoo ambapo Novemba 7, mwaka jana Yanga ilionekana kuwa salama kwa kipindi chote cha mchezo mpaka pale Lamine alipotolewa mapema kipindi cha pili kutokana na majeraha ya goti na Simba kusawazisha bao la kuongoza la Michael Sarpong.