NYOTA wa Yanga Jesus Moloko kwa sasa yupo zake DR Congo pamoja na beki Djuma Shaban ambao wote wameanza kuonyesha makeke yao ndani ya Ligi Kuu Bara.
Pia waliweza kucheza mchezo wa ufunguzi wa Ligi Kuu Bara ule wa Ngao ya Jamii, Septemba 25, Uwanja wa Mkapa na ubao huo ulisoma Simba 0-1 Yanga na bao lilipachikwa na Fiston Mayele.
Wachezaji hao wawili wamerejea kwao kupata pasi mpya za kusafiria baada ya zile za awali kujaa kwa mujibu wa ripoti kutoka ndani ya Yanga.
Taarifa imeeleza kuwa wakikamilisha suala hilo watarejea kambini kwa ajili ya maandalizi ya mechi za Ligi Kuu Bara na mchezo wao ujao utakuwa dhidi ya KMC ya Dar.
“Wachezaji wetu wanafuatilia pasi ili waweze kuendelea kuwa ndani ya Yanga na wakimaliza watarejea kuendelea kutimiza majukumu yao.Kuhusu sehemu ambayo kambi itawekwa hilo lipo mikononi mwa Kocha Mkuu, Nasreddine Nabi,” ilieleza taarifa hiyo.
Awali Nabi alieleza kuwa kikosi hicho kina mpango wa kuweka kambi Arusha kwa muda huu ambapo ligi imesimama.
Mchezo wao wa ligi wa Yanga utachezwa Songea Oktoba 19.