ILIKUWA Jumatatu timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars iliweza kuingia kambini kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wao wa kufuzu Kombe la Dunia.
Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mkapa, Oktoba 7 itakuwa dhidi ya Benin na kila timu inahitaji kushinda hivyo wachezaji wa Stars mna kazi ya kufanya.
Tayari mazoezi yalianza jana Oktoba 4 ambapo program zimeanza na hayatakuwa ya muda mrefu kwa kuwa muda uliobaki ni mfupi pia.
Ikumbukwe kwamba ni 2022 michuano hiyo inatarajiwa kufanyika Qatar hata kama Stars mnaongoza kundi J lazima mpambane kufanya vizuri.
Kazi ya nyumbani ikiisha sasa itakuwa ugenini ambapo huko imekuwa ni ngumu kwa Stars kupata ushindi kinachotakiwa sasa ni kuanza kumaliza kazi kwanza nyumbani kisha ugenini kuangalia namna itakayokuwa kwa kuchagua matokeo kulingana na kile ambacho kimepatikana Uwanja wa Mkapa.
Kuongoza kundi J kwa sasa haina maana kwamba timu imefanikiwa kufuzu bado kazi inaanza na lolote linaweza kubadilika ikiwa hakutakuwa na mapambano ya kweli.
Rai yangu kwa wachezaji wote ambao mmeitwa na kuanza mazoezi mjitume na kuonyesha kile ambacho mmepewa na Mungu pamoja na juhudi isiyo ya kawaida ndani ya uwanja.
Imani yetu ni kwamba wale ambao wameitwa na Kocha Mkuu, Kim Poulsen wanatambua kwamba wanakazi ya kuipeperusha bendera ya Tanzania.
Ili kuweza kufanya vizuri ni muhimu kupambana bila kuchoka kwani mechi hizi mbili zitakuwa na picha ya kile ambacho kinahitajika.
Mashabiki jambo ambalo wanahitaji kuona linatokea ni matokeo chanya hivyo kilicho cha msingi kwa muda huuu ni kila mchezaji kuweza kuona anapambana kwa hali na mali.
Ipo wazi kwamba Watanzania wana imani na wachezaji na wanajua kwamba mtafanya vizuri kusaka matokeo na iwe hivyo bila kuogopa.
Kila la kheri kwa maandalizi ya mwisho na tunaamini kwamba ile ndoto ya kuweza kufuzu itatimia na kila kitu kitakuwa sawa.
Kwa sasa ni zamu ya Stars kuonyesha kwamba kazi inaendelea na sio mahali pengine bali uwanjani.
Imeandikwa na Dizo_Click.