MATAJIRI wa Dar es Salaam, Klabu ya Azam FC imeweka wazi kuwa ipo tayari kwa ajili ya mchezo wao wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Pyramid FC ya Misri.
Mchezo huo wa kukata na shoka utachezwa bila ya uwepo wa mashabiki kutokana na maelekezo kutoka Shirkisho la Soka Afrika, (Caf) kwa sababu ya suala la Corona.
Ofisa Habari wa Azam FC, Zakaria Thabit amesema kuwa matarajio makubwa kwa timu hiyo ni kufanya vizuri kwenye kila mchezo ambao watacheza kutokana na uwepo wa wachezaji wazuri pamoja na benchi la ufundi makini.
“Azam FC tupo tayari kwa ajili ya ushindani, baada ya kuweza kushinda mechi zile za awali sasa tupo kwenye hatua nyingine ambayo tunatambua kwamba itakuwa ngumu na ushindani ni mkubwa.
“Kikubwa ni kuweza kuona tunapata matokeo kwani ipo wazi kila timu ambayo inaingia uwanjani inahitaji ushindi nasi pia tunahitaji kushinda,” amesema.
Kikosi cha Azam FC kimeendelea na mazoezi kwa ajili ya mchezo huo kwenye viunga vyao pale Azam Complex.
Miongoni mwa nyota ambao wapo kwenye kikosi hicho ni pamoja na Yvan Mballa na Idris Mbombo.