LAZIMA kichwa cha Didier Gomes kwa sasa kiwe kinapasuka kwa sababu mastaa wake wote nao ni pasua kichwa kutokana na mwendo wao ulivyo pamoja na mechi ambazo zipo mbele yake.
Gomes anakibarua cha kutetea taji la Ligi Kuu Bara ambalo Simba ilitwaa msimu uliopita wa 2020/21 pia ana kazi ya kuhakikisha kikosi hicho kinaweza kutinga hatua ya robo fainali Ligi ya Mabingwa na zaidi ya hatua hiyo ila sasa mastaa wake wameanza tofauti kabisa msimu huu.
Hii ni alama mbaya ikiwa hali itaendelea kuwa namna hii na majanga yakaendelea lazima Gomes achange karata vizuri huku akivuta picha kwamba kwa sasa hana nyota wake wawili ambao ni Clatous Chama na Luis Miquissone waliokuwa ni wachezaji muhimu pia kikosi cha kwanza.
Spoti Xtra ilipata nafasi ya kuzungumza na Gomes ili kujua kuhusu hesabu zake pamoja na namna ambavyo anawatazama wachezaji wake hao ilikuwa namna hii:-
Sadio Kanoute
Nyota huyu ingizo jipya ndani ya kikosi cha Simba mwenye umri wa miaka 24 ni raia wa Mali na alitambulishwa rasmi Agosti 20.
Eneo la kati lilianza kupata ile huduma iliyokuwa ikitolewa na Clatous Chama ila ghafla kwa sasa yupo kwenye ishu ya kutibu majeraha yake.
Aliumia kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga, Septemba 25 kwa sasa yupo kwenye program maalumu ili aweze kurejea kwenye ubora wake. Gomes amesema kuwa ni moja ya wachezaji wazuri eneo la kati hivyo anaamini kwamba atarejea kuwapa kile ambacho wanakihitaji.
Sakho
Alikutana na kashikashi za wababe ilikuwa Uwanja wa Jamhuri, Dodoma Oktoba Mosi wakati Simba ikisepa na ushindi wa bao 1-0 alipata maumivu ya mguu.
Ingizo hilo jipya ambalo lilitambulishwa Agosti 14 kutoka Tenghueth ya Senegal ikiwa hatakuwa imara kwa wakati huu kuna hatihati ya kuwakosa Wabotswana kwenye mchezo wa kwanza.
Gomes ameliambia Spoti Xtra kuwa nyota huyo amekuwa na uwezo wa kipekee hasa katika maamuzi na uwezo wa kupiga pasi.
Chris Mugalu
Nyota huyu ni chaguo namba moja kwa Kocha Mkuu, Didier Gomes kwa upande wa washambuliaji ambapo kwa sasa bado hajawa fiti kwa asilimia 100 baada ya kupata maumivu kwenye mchezo wa ligi uliopita dhidi ya Dodoma Jiji.
Gomes amesema kuwa kuhusu Mugalu ni aina ya washambuliaji ambao wana uwezo wa kumiliki mpira na kutoa pasi kwa usahihi.
“Ikiwa utahitaji kumzungumzia Mugalu ni aina ya mchezaji ambaye ana uwezo mkubwa wa kumiliki mpira na kutoa pasi. Ikumbuke ila pasi bora aliyotoa kwa Kagere, (Meddie) pale Dodoma.
Shomari Kapombe
Mzawa huyu naye bado yupo kwenye majanga ya kusumbuliwa na majeruhi ambapo aliumia kwenye mchezo wa kwanza wa ligi dhidi ya Biashara United.
Amekuwa ni pasua kichwa kwa Gomes kwa kuwa anatarajiwa kuwa nje kwa muda kidogo.
Gomes amesema:”Kapombe tunahitaji kuwa naye kwani ni moja ya wachezaji wazuri ila kwa sasa bado hajatengamaa kuwa imara tunatarajia hali yake itarejea kwenye ubora hivi karibuni.
Jeremiah Kisubi
Ameanza kwa mguu wa kushoto licha ya kufanya vizuri kwenye mazoezi ila hana nafasi ya kuanza kikosi cha kwanza kwa kuwa ni mgonjwa.
Huyu ni mlinda mlango namba tatu mali ya Simba ambapo msimu uliopita alikuwa anakipiga Tanzania Prisons.
Gomes ameliambia Spoti Xtra kuwa:”Kisubi ni kipa mzuri na anaonyesha uwezo mkubwa lakini anahitaji muda kwa kuwa alikuwa anaumwa, lakini kwa upande wa makipa naweza kusema wapo makipa wazuri ndani ya Simba ikiwa ni pamoja na Aishi Manula ambaye ni kipa anayecheza pia timu ya taifa.
Joash Onyango
Waziri wa ulinzi, mkali wa kazi zote chafu uwanjani, Joash Onyango huyu aliumia kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga, Uwanja wa Mkapa.
Asilimia zake ni chache kuweza kuanza kikosi cha kwanza kwa sasa kwa kuwa amekosekana kwenye mechi mbili za ligi ile ya Biashara united pamoja na Dodoma Jiji.
Kesi maalumu
Bernard Morrison, ninja huyu mzee wa kukinukisha muda wowote ule, alifungiwa mechi tatu kutokana na kitendo chake kilichotafsiriwa kuwa ni utovu wa nidhamu kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho, Kigoma.
Aliwakosa mabosi zake wa zamani Yanga kisha Biashara United na Dodoma Jiji kwa sasa adhabu yake imeisha sasa hilo neno la Gomes kuhusu Morrison sikia:”Morrison alikuwa na adhabu hivyo sikumtumia kwenye mechi tatu zilizopita, kuhusu kuanza kwa mechi zijazo hilo litafahamika wakati ukifika,” anamaliza Gomes kuhusu nyota wake.