YANGA imerejea Dar es Salaam juzi ikitokea Songea ilikoshinda mechi yake ya tatu dhidi ya KMC na kukaa kileleni. Kaimu Mtendaji Mkuu wa Yanga, Senzo Mazingisa amesisitiza kwamba hawabahatishi wana mpango kazi imara.
“Nafikiri waliokuwa na wasiwasi na Yanga hii watagundua kwamba kikosi chetu kipo katika ubora mkubwa, hatushindi kwa kubahatisha tunaonyesha ubora mkubwa ndani ya uwanja,” alisema Senzo ambaye ni raia wa Afrika Kusini aliyewahi kuwa Mtendaji Mkuu wa Simba.
Senzo alisema katika mechi zao tatu za Ligi Kuu Bara licha ya kushinda lakini idara ya ushambuliaji imefunga mabao, kiungo kina ubora wa kuzuia na kutengeneza mashambulizi.
“Timu imefunga mabao manne katika mechi tatu na mabao hayo yamefungwa na washambuliaji na viungo lakini ukiangalia hata safu ya kiungo inatengeneza nafasi vizuri bila presha hii ndio timu ambayo tunaitaka.
“Hatujaruhusu bao mpaka sasa, kuna ubora ambao wanao walinzi wetu, angalia kipa wetu Diarra (Djigui) na mabeki wote, nafikiri kuna heshima ambayo tunastahili kupewa mtu anapoizungumzia Yanga na sio kuona kama tunabahatisha,” alisema
“Tuna tofauti ukiangalia hata msimu uliopita tulianza ligi kwa kasi kubwa lakini baadaye mwishoni tukapungua kasi tukakosa ubingwa, msimu huu tofauti tumeanza taratibu kidogo na kulikuwa na sababu ila muda unavyosogea tunazidi kuwa bora zaidi,” alisema.