Hatma ya kocha Didier Gomes ndani ya Simba imezidi kuwa ya utata baada ya kukosekana katika mazoezi ya timu hiyo jana Jumatatu, Oktoba 25.
Simba jana jioni ilifanya mazoezi Uwanja was Boko Veterani ikiwa ni siku moja baada ya timu hiyo kupata matokeo ya kushtua wakipoteza nyumbani dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana kwa mabao 3-1.
Kipigo hicho ni cha kwanza kwa Simba kupoteza nyumbani katika mashindano ya Afrika tangu mwaka 2013 walipopoteza mara ya mwisho dhidi ya FC Libolo ya Angola.
Mbali na Gomes pia kocha wa makipa Milton Nienov pamoja na kocha wa mazoezi ya viungo Adel Zrane nao walikosekana katika mazoezi hayo.
Taarifa zinadai watatu hao walikuwa katika kikao na mabosi wa juu wa klabu hiyo kikao ambacho kilianza jana mchana.
Kocha Thieney Hitimana ndiye aliyeiongoza Simba katika mazoezi hayo ya jana wekundu hao wakijiandaa na mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya vinara wa Ligi Polisi Tanzania utakaopigwa Uwanja wa Mkapa Oktoba 27.
Kumekuwa na uvumi kwamba mpaka kufika leo Gomes huenda akawa sio kocha tena wa Simba hatua ambayo imetokana na kipigo hicho kutoka kwa Galaxy ambacho kimewaondoa wekundu hao katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika huku wakiangukia Kombe la Shirikisho Afrika