KIUNGO mshambuliaji mpya wa Simba, Ousmane Pape Sakho amerejea mazoezini pamoja na wachezaji wenzake baada ya kupona jeraha la mguu huku akipewa mazoezi maalum ya fitinesi.
Kiungo huyo ni kati ya wachezaji waliosajiliwa na timu hiyo katika kujiimarisha na Ligi ya Mabingwa Afrika na Ligi Kuu Bara.
Nyota huyo alikuwa nje ya uwanja akiuguza maumivu ya misuli aliyoyapata katika mchezo wa ligi dhidi Dodoma Jiji FC uliochezwa Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
Akizungumza na Championi Jumatatu, aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mfaransa Didier Gomes alisema kuwa kiungo huyo amepona majeraha yake huku akifanya mazoezi chini ya uangalizi wa daktari.
Gomes alisema kuwa kiungo ameanza na mazoezi hayo binafsi kwa hofu ya kujitonyesha ili asirejee katika majeraha yake hayo.
“Sakho amepona majeraha yake ya misuli na hivi sasa yupo chini ya uangalizi wa madaktari wa timu ili kuhakikisha anakuwa fiti zaidi.
“Hiyo ni baada ya kumuona hayupo fiti, hivyo kwa kuanzia anafanya mazoezi ya fiziki ili kuhakikisha anakuwa fiti zaidi. “inaamini kama akiwa fiti kwa asilimia mia moja, basi Sakho atakuwa msaada mkubwa katika timu,”alisema Gomes ambaye leo hii amefutwa kazi .