Afisa Habari wa Yanga,Haji Manara amesema kuwa licha ya kutambua ubora wa Azam FC lakini anaamini kuwa kikosi cha Yanga kina uwezo mkubwa wa kuondoka na ushindi mbele ya Azam FC.
Yanga Oktoba 30, katika Uwanja wa Benjamini Mkapa watakuwa na kibarua cha kucheza na Azam FC huku wakiwa na kumbukumbu ya kupoteza kwa bao 1-0 walipocheza na timu hiyo katika mchezo wa mwisho wa ligi kukutana ambapo ilikuwa msimu uliopita.
Manara alisema kuwa kuelekea katika mchezo huo wanafahamu kuwa utakuwa ni mchezo mgumu kwao lakini anaamini kuwa ubora wa kikosi cha Yanga utaenda kukipa ushindi dhidi ya Azam FC.
“Tunatambua ubora wa Azam katika ligi kuu ni timu nzuri lakini hilo halitufanyi sisi tushindwe kupata matokeo mbele yao, Yanga kwa sasa tunatimu bora ya kucheza na timu yeyote na tukapata ushindi hivyo tunatarajia kupata ushindi mbele ya Azam FC,”alisema Manara.
Yanga kwa sasa ndiyo vinara wa ligi kuu wakiwa wanaongoza ligi hiyo kwa pointi tisa mara baada ya kushinda katika michezo yote mitatu waliyocheza.