Home Azam FC AZAM FC YAKAMATWA NA POLISI TANZANIA

AZAM FC YAKAMATWA NA POLISI TANZANIA


AZAM FC leo Oktoba 2 imepoteza kwa kufungwa mabao 2-1 baada ya kukamatwa na Klabu ya Polisi Tanzania kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Uwanja wa Ushirika, Moshi.

Vijana hao wanaonolewa na Kocha Mkuu, George Lwandamina walianza kuokota nyavuni bao la kwanza dakika ya 23 kupitia kwa Kassim kisha lilisawazishwa na nyota wao Idd Seleman, ‘Nado’ dakika ya 29.

Ngoma kabla haijaenda mapumziko ingizo jipya la Polisi Tanzania, Adam Adam alipachika bao la pili dakika ya 40 na kufanya ubao wa Uwanja wa Ushirika kusoma Polisi Tanzania 2-1 Azam FC.

Dakika 45 za kipindi cha pili milango ilikuwa migumu kwa timu zote mbili kuweza kuongeza bao huku Polisi Tanzania wakifanikiwa kulinda ushindi wao.

Unakuwa ni mchezo wa kwanza kwa Azam FC kupoteza kwa msimu wa 2021/22 baada ya ule wa awali mbele ya Coastal Union kugawana pointi mojamoja baada ya kufungana bao 1-1.

Sasa Azam FC ni nafasi ya 10 kwenye msimamo ikiwa na pointi moja vinara ni Polisi Tanzania wenye pointi sita na mabao manne wanafuatiwa na Yanga walio nafasi ya pili na pointi sita wakiwa na mabao mawili.

Geita Gold imejichimbia nafasi ya 16 baada ya kupoteza mechi zake zote mbili za mwanzo.

SOMA NA HII  NKANE NA MAKAMBO WAFUFUKIA MAZOEZINI YANGA WAKIMPIGA MTU 8-0....CHICO USHINDI KAMA KAWAIDA 'KAZUBAA'....