Home news KOCHA YANGA AKIRI KUWA KUNA TATIZO KWENYE SAFU YA USHAMBULIAJI

KOCHA YANGA AKIRI KUWA KUNA TATIZO KWENYE SAFU YA USHAMBULIAJI


 KOCHA Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi amekiri kuwa ni kweli safu yake ya ushambuliaji inayoongozwa na washambuliaji Fiston Mayele na Heritier Makambo, imekuwa na tatizo la kukosa umakini na kupoteza nafasi nyingi za wazi na kuahidi kuwaandalia programu maalum ya kuhakikisha wanafunga mabao mengi zaidi.


Yanga Jumamosi walifanikiwa kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Geita Gold, katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliofanyika kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, ushindi ambao umewafanya kufikisha pointi sita na kuwaweka kwenye nafasi ya pili ya pili.


Licha ya ushindi huo, Yanga wameonekana kuwa na shida katika safu yao ya ushambuliaji ambapo katika michezo hiyo mitatu dhidi ya Simba, Kagera Sugar na Geita Gold wamefunga mabao matatu tu, bao moja kwenye kila mchezo.

Akizungumza  na Championi Jumatatu, Nabi alisema: “Tulikuwa na mchezo mzuri dhidi ya Geita Gold na kufanikiwa kupata pointi tatu muhimu, kwangu nawapongeza sana wapinzani wetu kwa ushindani waliotuonyesha.


“Licha ya ushindi huo lakini ni wazi bado tuna changamoto katika safu yetu ya ushambuliaji hasa kutokana na nafasi nyingi za mabao tulizokosa, lakini tumechukua changamoto hiyo na tutalifanyia kazi naamini katika michezo ijayo tutafunga mabao mengi zaidi.


“Kuhusu kwa nini Makambo anaanzia benchi naweza kusema tuna washambuliaji watatu wazuri na kwa sasa tunaanza na Fiston Mayele lakini naamini muda utafika Makambo na Yusuph Athumani watapata nafasi.”


Kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii uliochezwa Uwanja wa Mkapa ni Fiston Mayele aliweza kufunga bao la ushindi baada ya kutumia pasi ya mzawa Farid Mussa.


SOMA NA HII  BAADA YA KUMTAZAMA NGUSHI MAZOEZINI..NABI AKUNA KICHWA WEE...KISHA AIBUKA NA KUSEMA HAYA...