Home news WAGHANA KUWAFUATA MASTAA WA YANGA

WAGHANA KUWAFUATA MASTAA WA YANGA


YANGA ipo katika mazungumzo ya mwisho na Klabu ya Asante Kotoko ya Ghana itakayokuja nchini kucheza mchezo wa kirafiki.

Mchezo huo ni maalum kwa ajili ya kuwaandaa wachezaji wao wakati Ligi Kuu Bara ikiwa imesimama kupisha michezo ya kufuzu Kombe la Dunia mwaka 2022.

Mechi hiyo itawahusisha wachezaji waliobakia katika kikosi hicho wakiwemo Wakongomani Yannick Bangala, Fiston Mayele na Heritier Makambo.

Mmoja wa mabosi wa Yanga, ameliambia Championi Jumatano, wapo katika mazungumzo na timu mbili kutoka nje ya nchi zitakazokuja nchini kucheza michezo ya kirafiki.

Bosi huyo alisema kuwa kati ya timu hizo mbili mojawapo ni Kotoko ambayo bado hawajathibitisha kuja nchini huku wakitafuta nyingine.

Aliongeza kuwa lengo la kucheza michezo hiyo ya kirafiki ni kuwatengenezea fitinesi na muunganiko wachezaji wao ili ligi itakapoanza timu iwe imara tayari kwa ushindani.

“Bado Kotoko hawajathibitisha ujio wao hapa nchini kwa ajili ya kuja kucheza mchezo wa kirafiki, licha ya kuwapa taarifa na kuonyesha nia ya kukubali kuja.

“Mazungumzo yanakwenda vizuri hivi sasa na kama wakithibitisha kwa haraka, basi tutatangaza rasmi mchezo huo wa kirafiki tutakaoucheza kama siyo Arusha basi Dar.

“Pia uongozi upo katika mazungumzo ya mwisho na moja ya timu kubwa kutoka nje ya nchi itakayokuja nchini kucheza mchezo wa kirafiki, kwani kocha ameomba michezo miwili ya kirafiki pekee.”

Akithibitisha hilo, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Yanga, Hassani Bumbuli alisema kuwa: “Ni kweli kocha ameomba michezo miwili ya kirafiki ya kimataifa.

“Michezo hiyo ameiomba kwa ajili ya kutumia vema muda huu ambao ligi imesimama kutengeneza fitinesi na muunganiko wa timu, kuhusu timu tutakayocheza nayo tutaiweka wazi hivi karibuni.”


SOMA NA HII  NABI SIWAOGOPI WAARABU...KUWENI WAPOLE NIWANYOOSHE...TUMEPATA SIRI ZAO