MABOSI wa Simba wajanja sana. Baada ya kuangalia rekodi zao kwa misimu minne mfululizo na ishu za makocha kutoka Ulaya, sasa wameamua kubadilika na kuwapigia hesabu wale wanaotoka Afrika, lakini wakapewa mchongo na Kocha wa Al Ahly, Pitso Mosimane.
Mosimane aliyewahi kuifundisha na kuipa mafanikio Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, baada ya kusikia Simba imeachana na Didier Gomes, aliwatwangia simu na kuwapa jina la kocha anayewafaa.
Simba ipo katika mchakato wa kutafuta kocha mpya wa kuziba nafasi ya Gomes aliyeondokahivi karibuni baada ya kushindwa kuipeleka timu kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Jopo maalumu linalosimamia mchakato wa kupata kocha mpya limepokea wasifu (CV) za makocha kibao wanaotoka maeneo mbalimbali na wengi wao wakiwa ni Wazungu huku Waafrika wakiwa wachache.
Gazeti la Mwanaspoti limenukuu taarifa kutoka ndani ya jopo linalosimamia mchakato huo kuwa kocha msaidizi wa Mamelodi Sundowns, Rhulani Mokwena (34) ndiye anapewa nafasi kubwa ya kuchukua nafasi hiyo.
Kiongozi wa juu na mwenye maamuzi ndani ya Simba, alisema walipokea simu kutoka kwa kocha mkubwa Afrika (Al Ahly ya Misri), Pitso Mosimane na kuwapatia Mokwena na kuwaeleza atawafaa katika mahitaji yao, ingawa mchakato utaamua nani aje kumrithi Gomes.
Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez alipoulizwa na Mwanaspoti alisema katika orodha ya makocha waliyonayo wengi ni Wazungu, ila wao wanataka kocha wa Kiafrika anayejua utamaduni wa soka la Afrika pamoja na kukuza soka la Afrika.
“Suala la kocha halihitaji kukurupuka, kwani tunaweza kumpata mwenye wasifu mkubwa lakini akashindwa kutibu matatizo yaliyopo katika kikosi cha Simba na shida ikabaki pale pale,” alisema Barbara na kuongeza;
“Kama atakuwa Mokwena au mwingine hilo litajulikana ndani ya muda mfupi, lakini malengo ya klabu ni kumpata kocha kutoka Afrika na si Mzungu kama iliyetoka;
Barbara alifafanua; “Tunaweza kumpata kocha wa Afrika ambaye tunamuhitaji na wasifu wake usiwe mkubwa na akaweza kuisaidia timu kufikia malengo yake kwani atakuwa na kiu ya mafanikio na tutadumu naye kwa muda mrefu.
“Angalia klabu kama Chelsea wakati wanamchukua Thomas Tuchel wengi hawakuwa na imani naye, ila baada ya muda mfupi ameifanya timu kucheza vizuri na kushinda ubingwa wa Ulaya.”
Kwa misimu minne mfululizo Simba imekuwa na makocha kutoka Ulaya, Patrick Aussems, Pierre Lechantre, Sven Vandenbroeck na Gomes na misimu yote imebeba mataji ya Ligi Kuu Bara. Mara ya mwisho Simba kunolewa na Kocha Mkuu wa Kiafrika ilikuwa kipindi ikiwa na Joseph Omog.
Mokwena amekuwa msaidizi Mamelodi, Orlando Pirates na Chipa United ambako hakudumu