HII sasa sifa! ndivyo unavyoweza kusema kufuatia kauli ya kocha mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi ambaye ameweka wazi kuwa ubora wa sasa wa Yanga ni asilimia 45 tu ya kile anachokitaka, na baada ya muda watakuwa na timu ya kutisha zaidi.
Yanga Jumamosi iliyopita wakiwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam, waliendelea kasi yao ya ushindi baada ya kuichapa Azam FC mabao 2-0 katika mchezo wa mzunguko wa nne wa Ligi Kuu Bara.
Kutokana na ushindi huo Yanga imezidi kujiweka kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu wakiwa na pointi zao 12, katika michezo minne waliyocheza.
Akizungumza na gazeti la Championi Jumatatu, kocha Nabi alisema: “Kwanza nawapongeza sana wachezaji wangu kwa kuonyesha uwezo mzuri kwenye mchezo dhidi ya Azam, tumepata ushindi dhidi ya timu bora lakini licha ya ushindi huo na ubora tulionao naweza kusema kwa sasa timu yetu inacheza kwa asilimia 45 au 50 pekee ya kile nachohitaji.
“Mwanzoni mwa msimu huu niliomba miezi mitatu kutengeneza kikosi, na nikuhakikishie kuwa kwa mwenendo tuliaonao baada ya mwezi mmoja tutakuwa na kikosi kitakachotisha zaidi.
“Malengo yetu makubwa ni kushinda ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu na kwa usajili wa wachezaji na benchi bora la ufundi ambao umefanyika kwa udhamini wa GSM naamini tutafanikisha lengo hilo.”