Home news BAADA YA KUITWA STARS..REDONDO ASHINDWA KUJIZUIA..AFUNGUKA HAYA..ATANGAZA KUSTAAFU SOKA…

BAADA YA KUITWA STARS..REDONDO ASHINDWA KUJIZUIA..AFUNGUKA HAYA..ATANGAZA KUSTAAFU SOKA…


HABARI ya mjini kwa sasa ni kujumuishwa kwa kiungo mkongwe, Ramadhan Chombo ‘Redondo’ kwenye kikosi cha Taifa Stars, huku baadhi ya wadau wakibaki na maswali juu ya mchango wa nyota huyo na ushindani utakavyokuwa.

Redondo ambaye alizaliwa 1987, amekuwa na uwezo mkubwa tangu aanze kuitumikia Biashara United msimu uliopita ambapo kiwango chake kinashawishi zaidi msimu huu.

Mkongwe huyo ambaye alishazichezea timu kadhaa ikiwamo Azam FC, Simba hapa nchini, pia alishang’ara katika soka la kulipwa kwenye mataifa tofauti kama Afrika Kusini na sasa anakipiga Biashara United.

Vilevile alizitumikia Mbeya City, African Lyon kwa nyakati tofauti kabla ya kuibukia Biashara United waliomnasa kipindi cha dirisha dogo msimu uliopita ambao ameng’ara nao hadi sasa.

Kiungo huyo asiye na mambo mengi uwanjani, amefunguka kurejeshwa kwake Stars, huku akielezea ishu ya namba kikosini, matarajio na kutaja muda wake wa kutundika daruga.

KAZIKAZI UWANJANI

Redondo anasema siri ya kung’ara ni kutokana na maelewano mazuri ndani na nje ya uwanja kutokana na wachezaji wenzake kumheshimu, lakini naye pia anaiheshimu kazi yake.

Anasema anapokuwa uwanjani huwa anafikiria zaidi anachokifanya, huku akibainisha kuwa ubora wake mwingine ni kutokana na kujitunza vizuri mazoezini na kupata muda wa kupumzika.

“Huwa tunaheshimiana. Wao (chipukizi) kuna kitu wanapata, lakini hata mimi hupata faida kwao kwa sababu timu siyo ya mchezaji mmoja. Tunaelewana na kushirikiana, lakini napangilia vyema ratiba zangu,” anasema Redondo.

Nyota huyo mwenye mabao mawili Ligi Kuu Bara anaongeza kuwa, kuitwa kwake tena Stars sio kwamba anajua zaidi ya wengine, lakini amejipanga kuipa mafanikio nchi kama atabahatika kupangwa.

Anasema ushindani lazima uwepo kwani timu ya Taifa haiwezi kulinganishwa na klabu na kwamba, kuwa na uhakika wa namba Biashara United haiwezi kuamua moja kwa moja kikosini Stars.

“Biashara United ni tofauti kabisa na Stars, huku uhakika wa namba ninao, lakini Stars siwezi kujua itakavyokuwa. Kimsingi nimejipanga kuitumikia nchi yangu kwa mafanikio,” anasema nyota huyo.

SOMA NA HII  SIMBA YAWEKA MILIONI MIA NANE KWA USHINDI WA JPILI...BOSI AFICHUA ISHU YA MAYELE| SportXtra...

Hata hivyo, Redondo anawaomba wachezaji wenzake walioitwa Stars kujiandaa vyema na pia kukubaliana na uamuzi wa benchi la ufundi na kwamba atakayepata namba ahakikishe anaipigania timu hiyo.

Mchezaji huyo anaeleza kuwa kutokana na mwenendo alionao anafikiria kustaafu soka na kwamba, kwa sasa amejipa miaka mitano mbele kutundika daruga rasmi na kuanza maisha mapya nje ya soka.

Anasema licha ya watu wengi kumuona kama kazeeka si kweli, kwani alianza soka la ushindani akiwa bado mdogo na kilichompa jina kubwa mapema ni kutokana na kipaji alichomacho.

“Nimeanza mpira nikiwa mdogo. Kipaji kilinitambulisha mapema nikawa nacheza na mastaa pale Simba, kisha kwenda Azam, Mbeya City, Afrika Kusini lakini bado miaka mitano mbeleni nistaafu rasmi,” anasema Redondo.

AMKOSHA KOCHA

Akizungumzia kurejea Stars, Kocha Abdalah Mingange anasema licha ya umri wa nyota huyo kumtupa mkono, lakini anaweza kufanya vitu tofauti uwanjani kutokana na uwezo alionao.

“Nimemfundisha Redondo tukiwa Mbeya City, lakini 2008 tukiwa Taifa Cup pale Dar es Salaam niliona mapema uwezo wake. Sasa hivi ameisaidia Biashara United misimu miwili mfululizo, “ anasema Mingange.

“Sio huyo tu, bali hata Vitalis Mayanga anastahili kuwapo Taifa Stars.”