NAHODHA wa zamani wa Yanga, Papy Kabamba Tshishimbi aliyesajiliwa na timu ya Ligi ya Championship ya Kitayosce, amesema haoni shida kurudi tena Tanzania kucheza soka kwa vile hiyo ni kazi yake hata kama timu aliyosajiliwa ni ya daraja la chini, kwani anafurahia maisha ya Tanzania.
Tshishimbi aliondoka Yanga msimu wa 2018/19 baada ya kumaliza mkataba na timu hiyo na kurudi nchini kwao Congo ambako alijiunga na AS Vita aliyomalizana nao na akizungumza na gazeti la Mwanaspoti alisema ni kweli anarudi Tanzania kucheza Kitayosce na anatarajia kurudisha ubora wake.
“Narudi kweli na nimeshamalizana na hiyo timu, kazi yangu ni soka, siwezi kuchagua timu wala daraja la timu nitakayosajiliwa, naangalia maslahi kwanza,” alisema na kiungo huyo fundi wa mpira aliyewahi kukipiga Mbabane Swallows ya Eswatini kabla ya kutua Jangwani 2018.
“Nimefurahi kurudi tena Tanzania nikiwa na timu ya kucheza, bado niko katika ubora, naahidi kuisaidia timu yangu kufikia malengo ya kupanda daraja, natarajia ushindani wa kutosha lakini mipango ni kufanya vizuri,” alisisitiza kiungo aliyejizolea umaarufu kwa kuuwasha moto.
Tshishimbi alisema amefurahishwa na uongozi wa timu hiyo kuongeza nyota wenye uzoefu kikosini kwao na anaamini wamedhamiria kuona timu hiyo inapanda daraja na kusisitiza hawatawaangusha mashabiki wao.