KOCHA mpya wa Simba Pablo Franco ameanza kuyazoea maisha ndani ya timu yake hiyo mpya na ya kwanza kuitumikia Afrika, lakini ikielezwa ujio wake umewaweka njiapanda watukutu waliopo klabuni kwani jamaa anaelezwa hana utani kwenye ishu za utovu wa nidhamu.
Kocha Msaidizi wa Simba, Thierry Hitimana amedokeza kuwa, Pablo amewakalisha mastaa wa timu hiyo na kuwasihi kuzingatia nidhamu, kujituma, kufurahia uwepo wao Simba na kujua malengo ya timu kwa ujumla.
“Amewataka wachezaji kupigania jezi ya klabu, kujua mpira wa miguu ni maisha yao, kutobweteka na kujua kuwa wana uwezo mkubwa wa kuifikisha timu kwenye malengo ya kutwaa mataji,” alisema Hitimana na kumnukuu Pablo akisizitiza hatamchekea mchezaji atakayekuwa na nidhamu mbovu.
Alifafanua kuwa, kocha huyo wa zamani wa Getafe aliyewahi pia kuwa mchambuzi na msaidizi wa Real Madrid kwa siku 94 msimu wa 2018-2019 aliwaambia watakaoonyesha utovu wa nidhamu watapewa adhabu kulingana na makosa ambayo watakuwa wameyafanya.
“Pablo anaamini kuwa msingi wa mchezaji bora unaanzia kwenye nidhamu hivyo amewasihi kuzingatia hilo kwa manufaa yao wenyewe na ya klabu,” alisema Hitimana.
Hilo linajiri baada ya beki wa kimataifa wa Simba raia wa DR Congo, Henoc Inonga kupata kadi nyekundu kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa Oktoba 31, dhidi ya Coastal Union baada ya kumpiga kichwa Issa Abushehe.
Hitimana alisema ilikuwa ni msukumo wa mechi kwa beki huyo kufanya kitendo kisichokuwa cha kiungwana lakini baada ya kujua kuwa alifanya kosa aliomba radhi na uongozi ukamsamehe .
“Alilazimika kufanya hivyo kwa wachezaji na benchi nzima la ufundi lililokuwa sambamba na uongozi wa timu hiyo huku akiahidi kutofanya tena kosa kama hilo,” alisema.
Licha ya uongozi kumsamehe ila beki huyo alikumbana na adhabu kutoka kwenye kamati ya saa 72, baada ya kufungiwa mechi tatu na kutozwa faini ya Sh1 milioni.
Kati ya wachezaji ambao wamekuwa wakikumbana na adhabu ni Jonas Mkude.