LICHA ya wachezaji wote wa Yanga kuonekana moto wa kuotea mbali lakini Kocha wa viungo wa timu hiyo, ameweka wazi kwamba mastaa wawili wa DR Congo, Mukoko Tonombe na Fiston Mayele ndiyo wako fiti zaidi kimazoezi.
Helmy Gueldich ambaye ni Mtunisia kwenye mahojiano maalum na Gazeti la Mwanaspoti aliweka wazi kwamba kwamba mchezaji bora wa timu hiyo msimu uliopita Mukoko Tonombe sasa amerejea katika ubora wake baada ya hali ya kujiamini kurudi.
Helmy akafichua kwamba hata hivyo Mukoko ndio kiungo bora mwenye mapafu ya kazi ambapo kwa vipimo walivyofanya jamaa anaweza kukimbia kwa kilometa 20 kwa saa moja.
“Mukoko (Tonombe) sasa ameanza kurudi katika ubora wake ile hali ya kujiamini zaidi inarudi kwa kasi tofauti na tulivyoanza msimu lakini kuna kitu cha kipekee kwake ana mapafu mazuri anaweza kukimbia ni bora uwezo wake wa mapafu ni kilometa 20 kwa saa moja sasa huu ni ubora wa wachezaji ambao wanacheza hata Ulaya,”alisema Helmy
Helmy alisema faida kubwa ya ubora huo wa Mukoko ni kwamba anaweza kua mchezaji anayeweza kuwa na ubora wa kukimbia muda mrefu wa mchezo bila kuchoka ambapo kwa falsafa ya kocha wa timu hiyo Nesreddine Nabi atakuwa na msaada mkubwa.
“Faida kubwa ya hili anaweza kuwa katika ubora wa kuwa anakimbia muda wote ndani ya uwanja lakini pia linapokuja suala la kurudisha nguvu baada ya kazi nzito hii inamsaidia kutokana na ubora wa mwili wake,ndani ya uwanja anaweza kukimbia kwa haraka na hata taratibu,kwa ubora huu anaweza kukimbia haraka na akapumzika kwa sekunde tano mpaka saba kisha akawa na mikimbio mingine ya haraka.
Aidha Helmy alisema ubora huo pia upo kwa mshambuliaji Fiston Mayele ambaye amekuwa na nguvu za kutosha kupambana na mabeki. Alisema Mayele kama amemiliki mpira kwa nguvu zake ni vigumu kwa mabeki kumsumbua wakafanikiwa kuchukua mpira ubora ambao umewafanya makocha kumfanya chaguo la kwanza katika timu hiyo.
“Kuna Fiston Mayele huyu ana nguvu sana sio rahisi kuchukua mpira akiwa anaumiliki labda umuumize kwa mshambuliaji ni kitu kizuri kwa kuwa anapambana na mabeki ambao wengi wanakuwa na nguvu sana ila pia unamuona ana akili na utulivu mkubwa kwa ubora wake sishangai kwanini amekuwa chaguo la kwanza kwa kocha ni mshambuliaji aliyekamilika,”aliongeza Kocha huyo.