WAKATI watani wakijipanga kwa ajili ya michezo mingine ya Ligi Kuu Bara ukiwemo ule utakaowakutanisha wao Desemba 11, Uwanja wa Mkapa, kumekuwa na taarifa za madai ya benchi la ufundi la Yanga kutokuwa na mawasiliano mazuri ingawa Kaimu Mtendaji Mkuu Senzo Mazingisa amesema mashabiki wao wasivurugwe kwani ni taarifa tu za kuwatoa mchezoni.
Mara kadhaa timu hizo zikikaribia kukutana kwenye mechi za kimashindano huibuliwa mambo mengi ambayo sasa wanayanga wameambiwa wanapaswa kuwa watulivu kwani kwenye benchi lao amani imetalawa.
Akizungumza na Mwanaspoti, Senzo alisema hakuna taharuki yoyote ndani ya klabu yao kwa sasa na kila kitu kipo sawasawa na kama kuna kitu kinapikwa basi ni mipango ya kushinda mechi zao mbili zijazo dhidi ya Mbeya Kwanza na ile ya Simba.
Bosi huyo alisema anafahamu inapokaribia mechi dhidi ya Simba kuna mambo mengi huibuka lakini ziara aliyoifanya juzi kambini amegundua hakuna tofauti yoyote zaidi ya hesabu za kusaka ushindi tu.
Juzi iliibuka taarifa makocha wawili wa timu hiyo Nesreddine Nabi na msaidizi wake, Cedric Kaze hawapatani taarifa ambayo ilivuma na kuwashtua mashabiki wa Yanga.
“Hakuna hicho kitu nilishangaa zaidi hali ambayo nimeikuta jana (juzi) kambini kinachofanyika kule ni ushirikiano kwa watu wote ili tushinde hizi mechi mbili na zingine zijazo hakuna kingine unapoona hizi taarifa unalazimika kucheka kama nilivyofanya,” alisema Senzo.
“Nimekaa hapa Tanzania kwa muda mrefu sasa, nafahamu siasa za namna hii hasa wakati kama huu ambao unakaribia mchezo kati ya hizi klabu kubwa, kuna watu wanakuwa nyuma ya hizi propaganda nafikiri haziwezi kutuondoa katika tamaa ya kutaka ushindi na Yanga itashinda hizi mechi mbili na zingine zinazokuja.
“Unakaa wakati huu unaambiwa Aucho (Khalid) alisaini mkataba wa miezi sita unageukia huku unasikia makocha wanagombana kwa klabu kama Yanga unawezaje kuwa na mchezaji kama Aucho ukampa mkataba wa miezi sita hata wadhamini wetu hawawezi kufanya makosa ya namna hii,” alisema.
Senzo alisema ziara yake kambini amegundua kuna mbinu sahihi zinafanyiwa kazi kuhakikisha wanabadili upepo wa kurejea katika ushindi baada ya kupata sare ya kwanza katika mchezo wa mwisho dhidi ya Namungo ugenini.
Aliongeza amevutiwa na morali ya wachezaji ambao wanatamani ushindi mkubwa katika mechi ijayo sambamba na kurejea kwa wachezaji ambao walikuwa majeruhi.
“Tutaondoka kwenda Mbeya ndani ya siku mbili kutoka sasa (jana) nataka niwaambie mashabiki wa Yanga wachezaji wanataka sana ushindi wa hii mechi inayokuja na ile ya Simba, kila mchezaji ambaye alikuwa majeruhi amerejea.”