Home news BAADA YA KUKIONA KIKOSI CHA SIMBA…PABLO ‘AWAKATA MAINI’ WANAOTARAJIA MAFANIKIO YA HARAKAHARA...

BAADA YA KUKIONA KIKOSI CHA SIMBA…PABLO ‘AWAKATA MAINI’ WANAOTARAJIA MAFANIKIO YA HARAKAHARA …


Kocha Mkuu wa Klabu Bingwa Tanzania Bara Simba SC, Pablo Franco ameomba muda wa majuma matatu ili kikosi chake kiweze kucheza kwa ushindani katika mashindano wanayoshiriki msimu huu 2021/22.

Simba ndio Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara na Kombe la Shirikishi ‘ASFC’ huku wakitarajia kucheza dhidi ya Red Arrows ya Zambia kwenye hatua ya mtoano ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika ‘CAF’.

Pablo amesema tangu aanze majukumu ya kuifundisha timu hiyo ameshuhudia vipaji vya hali ya juu kwa wachezaji wake.

“Nafurahi kuona kazi yangu haitakuwa ngumu sana kutokana na uwezo walionao wachezaji niliowakuta hapa, bado nasubiri wale waliopo timu ya taifa nadhani wiki tatu zitatosha kutufanya kuwa bora,” amesema Pablo.

Kocha huyo kutoka nchini Hispania amesema kitu kikubwa ambacho anakifanya kwenye mazoezi ni kujenga muunganiko utakaofanya timu hiyo icheze kwa maelewano.

Amesema anajua falsafa ya klabu ya Simba ni kupiga pasi nyingi, na hilo anataka kuliongezea vitu ili liweze kunoga na kuwachanganya wapinzani wao kitu ambacho kitawasaidia kupata ushindi kirahisi.

Aidha, kocha huyo amesema kuelekea mchezo wao wa hatua ya mtoano wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Red Arrows anaendelea na maandalizi, huku akiwasoma wapinzani wao ili kujua mbinu zao.

Pablo amejiunga na Simba kwa mkataba wa miaka miwili akichukua mikoba ya Kocha kutoka nchinin Ufaransa Didier Gomes ambaye aliamua kuachia ngazi baada ya klabu hiyo kushindwa kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kufungwa na Jwaneng Galaxy ya Botswana.

Kazi ya kwanza ya Kocha Pablo inatarajiwa kuwa siku ya Ijumaa katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Ruvu Shooting utakaopigwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

SOMA NA HII  YANGA:TUTATWAA MATAJI YOTE MSIMU HUU