Home Habari za michezo UKWELI MCHUNGU… MASHABIKI SIMBA WANAPASWA KUJUA CHAMA SIO MKUBWA KULIKO KLABU..

UKWELI MCHUNGU… MASHABIKI SIMBA WANAPASWA KUJUA CHAMA SIO MKUBWA KULIKO KLABU..

Chama na Simba SC Msimu Huu

Kumekuwa na mjadala mkubwa kutoka kwa mashabiki wa soka nchini hususan wa Simba wakipinga na kumwona Kocha Mkuu mpya wa klabu hiyo, Robertinho Oliveira, hafai baada ya kufanya mabadiliko ‘sub’ na kumtoa Clatous Chama.

Robertinho ambaye katika mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu Bara akiwa na Simba Jumatano iliyopita, aliiongoza kushinda mabao 3-2 dhidi ya Mbeya City, alimtoa Chama dakika ya 31 ya kipindi cha kwanza na kumwingiza Pape Sakho.

Katika mechi hiyo iliyopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Chama alitolewa wakati huo matokeo yakiwa bao 1-1, huku akiwa mpishi wa bao hilo, jambo ambalo mashabiki wa Simba walizomea uamuzi huo uwanjani hapo.

Malalamiko hayo yaliendelea hata kwa mashabiki waliokuwa wakifuatilia mechi hiyo kupitia televisheni na kisha mjadala mkubwa kutawala vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Wengi wakidai haiwezekani Chama kutolewa kwa kuwa yeye ndiye mhimili wa timu na amekuwa akiibeba kutokana na maamuzi yake sahihi ambayo amekuwa akiyafanya uwanjani. Mashabiki hao wamefika mbali huku baadhi wakitaka atimuliwe.

Hata hivyo, mabadiliko aliyoyafanya Robertinho yalijibu baada ya muda mfupi tu kwani Simba ilipata bao la pili kwa mkwaju wa penalti iliyofungwa na Saido Ntibazonkiza kabla ya Sakho aliyechukua nafasi ya Chama kufunga la tatu.

Bao hilo la Sakho lilimuinua Robertinho aliyewageukia mashabiki uwanjani hapo na kushangilia kwa furaha kubwa, ikiwa ni ishara ya kuwaonyesha kwamba yeye ni kocha mwenye taaluma hiyo, hivyo hakufanya makosa kumtoa Chama.

Kwa ujumla mashabiki wa Simba wanapaswa kuelewa jambo moja kwamba kocha anapaswa kuachwa huru kuamua ni mchezaji gani wa kuanza, kutokea benchi na yupi anayestahiki kufanyiwa mabadiliko wakati wowote.

Kitaalamu kocha anapokuwa nje na wasaidizi wake ana akili ya kuusoma mchezo mzima na anapofanya mabadiliko anakuwa tayari ameona tatizo liliko katika kikosi chake na udhaifu wa wapinzani, hivyo kutoa maelekezo ya nini cha kufanya kwa mchezaji anayeingia.

Kadhalika, Chama si mchezaji mkubwa pekee anayeibeba timu yake katika ulimwengu wa soka, ambaye ameanza kufanyiwa mabadiliko, tumeshuhudia kwa nyakati tofauti Lionel Messi na Cristiano Ronaldo ‘CR7’ wakiwa kwenye ubora wao wakifanyiwa mabadiliko na timu zao kupata matokeo chanya kama iliyotokea kwa Simba katika mchezo huo.

Lakini ni mashabiki hao hao wa Simba ambao hivi karibuni kabla ya dirisha dogo la usajili kufunguliwa na kufungwa Januari 15, mwaka huu, walikuwa wakilalamika na kuutaka uongozi usajili kiungo mshambuliaji mwenye uwezo kama Chama ama zaidi yake.

Hiyo ilitokana na timu hiyo kuwa katika wakati mgumu wa kupata matokeo pindi Chama alipokuwa nje akitumikia adhabu ya kufungiwa michezo mitatu, hivyo uongozi uliliona hilo na kumsajili Ntibazonkiza.

Hivyo, alichokifanya Robertinho katika mchezo huo, sisi tunamwelewa kwani mbali na sababu nyingine zilizotolewa, ni wazi uamuzi wa kumtoa Chama alitaka pia kuona ni namna gani Ntibazonkiza anaweza kuibeba timu mabegani mwake pindi Chama akiwa hayupo.

Kwa mantiki hiyo mashabiki wa Simba na wapenzi wa soka kwa ujumla hawana budi kuheshimu taaluma za makocha wao, lakini kutambua Robertinho bado anaendelea kuwasoma na kujaribu kutambua uwezo wa kila mchezaji kulingana na mfumo wake, hivyo kuendelea kusema Chama hapaswi kutolewa hata kama akikosea ni kumvimbisha na kumfanya ashindwe kuheshimu maamuzi ya kocha.

SOMA NA HII  SIKU KADHAA KABLA YA SIMBA vs YANGA..REKODI HIZI ZITACHAFUA HALI YA HEWA..BOCCO HAONEKANI...