Home news KUELEKEA MECHI YA SIMBA VS YANGA..BODI YA LIGI WATIA NGUMU KUSOGEZA TAREHE...

KUELEKEA MECHI YA SIMBA VS YANGA..BODI YA LIGI WATIA NGUMU KUSOGEZA TAREHE MBELE…YANGA WATO NENO..


IMEBAKI kama mwezi mmoja kabla ya watani wa jadi nchini, Simba na Yanga kuvaana kwenye mechi yao ya kwanza ya Ligi Kuu Bara msimu huu itakayopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam, Desemba 11.

Hata hivyo, wakati mechi hiyo ikiwa jirani, Yanga inaonekana kuizidi ujanja Simba katika maeneo mawili ambayo pengine watani wao wasingependa iwe hivyo kabla ya mchezo huo utakaokuwa wa 107 kwa timu hizo kukutana ndani ya Ligi Kuu Bara tangu mwaka 1965.

Eneo la kwanza ni kutanguliwa kwao kwa tofauti na pointi nne baada ya michezo mitano ya kwanza, hivyo kama timu hizo mbili zitapata ushindi katika michezo ya ligi iliyobakia kabla ya kukutana maana yake Yanga itaingia uwanjani Desemba 11 ikiwa haina presha kubwa kwani matokeo yoyote itakayopata yataifanya iendelee kubakia kileleni.

Lakini ukiweka kando hilo, Yanga itaingia katika mechi hiyo ikiwa imepata muda mrefu na wa kutosha kujiandaa nao kulinganisha na Simba wanaokabiliwa na ratiba ngumu kutokana na ushiriki wake katika Kombe la Shirikisho Afrika.

Yanga itapata muda wa takriban siku 10 kujiandaa na mechi hiyo dhidi ya Simba kwani itacheza mechi yake ya mwisho kabla ya kuwavaa watani zao, dhidi ya Mbeya Kwanza, Novemba 30.

Wakati hali ikiwa hivyo kwa Yanga, Simba yenyewe itakuwa na siku tano tu za maandalizi zinazoweza kupungua zaidi ikiwa watakumbana na changamoto ya usafiri kwani wenyewe watacheza mchezo wao wa mwisho kabla ya kuivaa Yanga Desemba 5 ugenini huko Zambia utakaokuwa ni wa marudiano wa hatua ya mwisho ya awali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Red Arrows.

Changamoto hiyo ya muda mfupi wa maandalizi kuelekea mechi ya watani wa jadi, iliwakumba Yanga, Septemba, kwani Septemba 19 walikuwa na mchezo wa marudiano ugenini wa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Rivers United ya Nigeria.

Siku sita baadaye walikuwa na mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Simba iliyokuwa na muda mrefu wa kujiandaa kutokana na kutoanzia hatua hiyo ya awali, lakini hata hivyo waliibuka na ushindi wa bao 1-0.

SOMA NA HII  MTAMBO WA MABAO YANGA WAOMBA SAPOTI YA MASHABIKI, WAAHIDI KUPAMBANA

Mbali na muda mrefu wa maandalizi, Yanga pia ina faida nyingine ya wachezaji wake kupumzika vya kutosha kwani itacheza mechi mbili tu za ligi kabla ya kuivaa Simba na watakuwa na wastani wa kupumzika kwa siku 10 kutoka mchezo mmoja hadi mwingine.

Novemba 20 wataivaa Namungo na baada ya hapo itakaa siku 10 kabla ya kucheza na Mbeya Kwanza Novemba 30 kabla ya kuvaana na watani zao, ingawa vijana hao wa Jangwani mechi zao zote zijazo ikiwamo ya Simba wanachezaji wakiwa ugenini tofauti na watani wao wenye mseto tofauti.

Wachezaji wa Simba wenyewe watalazimika kucheza idadi ya mechi nne za Ligi na Kombe la Shirikisho zitakazowafanya wawe na siku chache za kupumzika kutoka mechi moja hadi nyingine.

Novemba 19, Simba itakuwa Mwanza kuvaana na Ruvu Shooting kisha itarejea Dar es Salaam kuikabili Red Arrows Novemba 28. Baada ya hapo siku nne baadaye itaikabili Geita Gold, Desemba Mosi na itasafiri hadi Zambia kwa mechi ya marudiano na Red Arrows, Desemba 5 ndipo itasalia na kibarua cha kuivaa Yanga mbele yake.

Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu (TPLB), Almas Kasongo alisema ratiba imezingatia kalenda ya kimataifa hivyo alisisitiza kuwa haitokuwa na mabadiliko.

“Wakati tunaandaa ratiba tulizingatia changamoto mbalimbali ikiwemo kalenda ya mashindano ya kimataifa hivyo sioni tatizo kwa ratiba iliyopo na hakuna mabadiliko yoyote kwa sasa,” alisema Kasongo.

Mkurugenzi wa mashindano wa Yanga, Thabit Kandoro alisema hawaiwazii mechi ya Simba kwa sasa.

“Kwa sasa akili yetu tumeielekeza kwenye mechi zetu mbili zilizo mbele dhidi ya Namungo na Mbeya Kwanza ambazo tunahitaji kuvuna pointi sita,” alisema Kandoro.