Home news SIMBA SC TABU IKO PALEPLE…..HIZI HAPA SIKU 61 ZA JASHO, MACHOZI YA...

SIMBA SC TABU IKO PALEPLE…..HIZI HAPA SIKU 61 ZA JASHO, MACHOZI YA DAMU..WAKIZINGUA IMEKULA KWAO….


SIMBA ina siku 61 mbele yake kabla ya mwaka kumalizika ambazo ikiwa itachanga vyema karata zake na kuvuka salama, itakuwa na nafasi kubwa ya kutetea ubingwa wake wa Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho la Azam pamoja na kufanya vizuri kimataifa.

Mchakato wa kurekebisha benchi lake la ufundi, ratiba ya mechi za kimataifa na ratiba ya mashindano ya ndani ni mambo matatu yanayofanya kipindi cha miezi miwili iliyobakia kiwe kigumu kwa Simba na kama itapenya vizuri katika vihunzi hivyo huenda msimu ukawa wa kicheko kwa mara nyingine kwa wapenzi na mashabiki wake.

MABADILIKO YA BENCHI

Changamoto ya kwanza kwa Simba katika muda huo ni zoezi la kumsaka kocha mkuu mpya atakayerithi nafasi iliyoachwa na Didier Gomes da Rosa ambaye wamefikia uamuzi wa kuvunja mkataba baada ya timu hiyo kutupwa nje ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Lakini sio tu mrithi wa Gomes bali pia Simba ndani ya muda huo italazimika kuziba mapengo ya aliyekuwa mtaalamu wa mazoezi ya viungo wa Simba, Adel Zrane na kocha wa makipa, Milton Nienov ambao nao wamefungishwa virago baada ya dhahama ya kutolewa katika Ligi ya Mabingwa na timu ya Jwaneng Galaxy ya Botswana.

Tayari uongozi wa Simba umeanza mchakato wa kupata warithi wa makocha hao kama ilivyothibitishwa na Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Klabu hiyo, Mulamu Nghambi.

“Makocha wengi wametuma CV zao. Miongoni mwao hao wawili waliowahi kuifundisha Simba na wanaijua vilivyo,” alisema Mulamu.

Kocha mpya wa Simba atahitaji siku chache za kukifahamu kikosi kiujumla na mchezaji mmojammoja na kisha kuanza kazi ya kurekebisha udhaifu uliopo kwa mujibu wa tathmini yake atakayoifanya kwa kikosi na kuimarisha maeneo ambayo timu inaonekana kuwa na ubora.

Udhaifu mkubwa ambao umeonekana katika kikosi cha Simba katika siku za hivi karibuni ni kukosa ubunifu wa kupenya safu ya ulinzi ya timu pinzani na pia kutengeneza nafasi nzuri za mabao jambo ambalo limeifanya kasi yake ya kufumania nyavu ipungue.

Lakini pia safu ya ulinzi ya Simba imekuwa na tatizo la kushindwa kuokoa mipira ya juu ambalo liliwagharimu dhidi ya Jwaneng Galaxy ambayo hata kocha wake Morena Ramaboli alifichua mara baada ya mchezo kumalizika.

“Tuliwatazama Simba na kuwafanyia tathmini tukagundua pindi wanaposhambuliwa kwa mipira ya juu wamekuwa wakiacha nafasi kati ya mlinzi na mlinzi hivyo nikawaelekeza wachezaji wangu wawe wanahakikisha wanakuwa kwenye ile nafasi jambo ambalo lilizaa matunda,” alisema Ramaboli.

SOMA NA HII  RASMI...UJIO WA KISINDA WAMUWEKA KANDO KAMBOLE...YACOUBA, MAKAMBO NA MOLOKO KUCHUNGUZWA...

KALENDA KIMATAIFA

Ukiondoa hilo, mambo mengine mawili magumu kwa Simba katika kipindi cha siku 61 zijazo ni kalenda ya mashindano ya kimataifa.

Novemba 28, Simba itakabiliwa na mchezo wa kwanza nyumbani wa kuwania kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Red Arrows ya Zambia na timu hizo zitarudiana Desemba 5 huko Zambia.

Lakini kocha mpya wa Simba huenda akakumbana na wakati mgumu katika maandalizi ya mechi hizo mbili dhidi ya Red Arrows kwani yataingiliwa na kalenda ya mechi mbili za mwisho za hatua ya makundi ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika Qatar mwakani kwa upande wa bara la Afrika.

Simba huenda ikawakosa wachezaji wake muhimu wa kikosi cha kwanza kwa muda wa wiki mbili za mwanzo za Novemba ambao watakuwa katika majukumu ya timu zao za taifa kwenye kipindi hicho.

Mechi za raundi ya tano ya hatua hiyo ya makundi ya kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia zitachezwa kati ya Novemba 11 hadi 13 na zile za raundi ya sita zitachezwa kati ya Novemba 14 hadi 16.

Ni kipindi ambacho Simba bila shaka watakuwa wakiombea nyota wao watakaokwenda katika majukumu ya timu za taifa wasipate majeraha ambayo yanaweza kuwagharimu katika mechi zao.

MASHINDANO YA NDANI

Ukiondoa kalenda hiyo ya mashindano ya kimataifa, Simba pia itakabiliwa na mechi saba za Ligi Kuu Bara na mchezo mmoja wa hatua ya 32 bora ya Kombe la Shirikisho la Azam.

Mechi sita ambazo itacheza za Ligi Kuu ni dhidi ya timu za , Namungo, Yanga na Geita ambayo itakuwa nyumbani na tatu dhidi ya Ruvu Shooting, Kagera Sugar na KMC itakuwa ugenini wakati mpinzani itakayekutana naye kwenye Kombe la Shirikisho la Azam, atajulikana baada ya droo itakayochezeshwa ya hatua hiyo.

Imeanza kulazimishwa sare na  Coastal Union, Jumapili, Oktoba 31 na baada ya hapo itacheza na Namungo FC, Novemba 3 kisha itakaribishwa na Ruvu Shooting, Novemba 19.

Baada ya hapo Desemba Mosi itacheza na Geita Gold kisha Desemba 11 itacheza na Yanga na itafunga mwaka kwa kukabiliana na Kagera Sugar, Desemba 18 na Desemba 24 itakabiliana na KMC.