UONGOZI wa timu ya Red Arrows ya Zambia, umeweka wazi wamepanga kulipa kisasi katika mchezo wa marudiano dhidi ya Simba licha ya kufungwa mabao mengi kutokana na mvua iliyoharibu hali ya uwanja na kukwamisha mipango yao.
Timu hiyo inayomilikiwa na Jeshi la Anga la Zambia, imepoteza mchezo wa kwanza wa Kombe la Shirikisho kwa mabao 3-0 dhidi ya Simba kabla ya mchezo wa marudiano unaotarajiwa kupigwa Jumapili ya Desemba 5 huko Zambia ambapo mshindi wa jumla ataenda makundi Shirikisho.
Akizungumza na Championi Jumatano, meneja wa timu hiyo Rio Flowers, alisema: “Tunaamini sasa ni wakati wa kulipiza kisasi cha kuhakikisha tunawaondoa kwa kuwafunga mabao mengi ili kuzidi yale ambayo wao wametufunga huko.
Ukweli tunawaheshimu kwa sababu ni timu bora lakini kwa upande wetu tunachotaka kukifanya ni kuhakikisha tunapata ushindi mkubwa hapa kwetu.”